Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), mkoa wa Mbeya, Emmanuel Kiabo amkamate na kumhoji aliyekuwa Meya wa jiji la Mbeya, Athanas Kapunga na wenzake 11 kwa tuhuma za kuisababishia Serikali hasara za bilioni 63.448.

Waziri Mkuu amesema watumishi hao wanatakiwa kuchukuliwa hatua stahiki za kisheria baada ya kusababisha hasara kubwa katika mradi wa ujenzi wa soko la Mwanjelwa, lililoko jijini Mbeya.

”Serikali hii hawezi ikawaachia watu hawa ambao wameisababishia hasara kubwa kiasi hiki tena kwa halmashauri moja. kama wako humu ndani, naagiza wakamtwe na wasakwe popote walipo ili nao waje kujibu hoja.”

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo Julai 31, 2017 wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri za Wilaya ya Mbeya na Halmashauri ya Jiji la Mbeya katika mkutano uliofanyika ukumbi wa Benjamini Mkapa.

Watuhumiwa hao ni pamoja na waliowahi kuwa wakurugenzi wa jiji hilo ni pamoja na Mussa Zungiza, Elizabeth Munuo, Juma Idd na Dkt. Samweli Lazaro aliyekuwa akikaimu nafasi ya ukurugenzi.

Watuhumiwa wengine pamoja na aliyewahi kuwa muweka hazina wa jiji, James Joroj pamoja na waliokuwa wajumbe wa Bodi ya zabuni ambao ni Mussa Mapunda, Samweli Bubengwa, Davis Mbembela, Lydia Herbert na Bernard Nsolo ambao walipitisha nyongeza ya mradi huo bila ya kuzingatia maslahi ya jiji pamoja na Emily Maganga ambaye hakuishauri vizuri bodi hiyo.

Pia, Waziri amesema mbali na kuzidisha kiasi cha mkopo hata baada ya kukamilika kwa ujenzi watuhumiwa hao walighushi mikataba ya upangaji jambo ambalo kinyume na matakwa na sheria ya Manunuzi ya umma.

Amesema kuwa vizimba viligaiwa kwa wafanyabiashara bila kufanya mchakato wa manunuzi, hivyo Waziri Mkuu ameagiza Mkuu wa Mkoa Mbeya, Amos Makalla akutane na madiwani wa Halmashauri ya jiji kuweka mikakati namna ambavyo watapanga bei ya vizimba katika soko hilo.

Video: Mdee aiponda bajeti ya Serikali
Tatizo la maji safi na salama kuwa historia nchini