Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameongoza wabunge katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma kuaga mwili wa aliyekuwa mbunge wa Dimani, Zanzibar, Hafidh Ally Tahir aliyefariki saa 9 alfajiri ya kuamkia leo katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kabla ya kusafirishwa kwenda Zanzibar kwa mazishi.

Akizungumza katika tukio hilo, Waziri Mkuu ametoa pole kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai, familia ya marehemu na wabunge wote. “Tumepokea taarifa za msiba huu kwa mshtuko mkubwa. Leo tupo katika wakati mgumu sana. Tumeondokewa na viongozi wengi,” amesema.

Majaliwa amesema wafiwa wanatakiwa kuishi kwa upendo. “Tumuombee marehemu, tuiombee familia iwe na moyo wa utulivu katika kipindi kigumu cha kuondokewa na mpendwa wao.”

Hafidh alizaliwa Oktoba 30, 1953 na aliwahi kuwa Mkuu wa Sauti ya Tanzania Zanzibar (1970-1978) na amekuwa mbunge tangu 2005 hadi mauti yanamkuta.

Enzi ya uhai wake, alishiriki kikamilifu katika masuala ya michezo, alikuwa mwamuzi wa soka mwenye beji ya FIFA na kocha msaidiizi wa timu ya soka ya Bunge na hadi jana, Hafidh alishiriki katika shughuli mbalimbali ikiwemo uchaguzi wa kupata viongozi wa Tawi la Umoja wa Wabunge WanaYanga mjini Dodoma ambapo yeye alichaguliwa kuwa Katibu.

Video: Waziri Mwakyembe amlilia Samuel Sitta Bungeni
Mmiliki wa Facebook afunguka kuhusu tuhuma za kumpandisha Trump