Na: Joseph ‘Josefly’ Muhozi

“Kivipi bro unatabiri hawatanipenda? Hakuna aijuaye kesho hata mtunzi wa kalenda.” Ni moja kati ya Nikki wa Pili kwenye ‘Niaje ni Vipi’.

Moja kati ya mijadala mikubwa iliyowasha moto kwenye mitandao ya kijamii hususan wiki hii ni tangazo la rapa  wa kundi la Weusi, Nikki wa Pili. Huyu ni Nickson mtoto wa Mzee Simon, mzaliwa wa jiji la Arusha aliyeweka wazi kuwa ana ndoto ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania!

Binafsi nilimfahamu Nikki kwa kumsikia kwa rafiki yangu aliyekuwa anasoma naye darasa moja chuo kikuu, shahada ya kwanza (under graduate). Alinieleza jinsi Nikki alivyokuwa hatari kwa mistari na kwamba alikuwa ‘anachana’ sana mbele ya kadamnasi, alimpa sifa nyingi kama msanii japo hakujulikana. Wakati huo Joh Makini ni moto tayari. Kwahiyo, nilipomsikia Nikki kwenye ‘Good Boy’, ‘Niaje ni Vipi’ tayari nilikuwa namtarajia, hakuni-surprise.

Lakini kwa upande mwingine, nazifahamu zaidi fikra za Nikki kupitia andiko lake la ‘Kalamu ya Nikki wa Pili’. Ni andiko ambalo lilikuwa linatoka kila wiki, na kwa bahati nzuri mimi nilikuwa nalipokea na kulihariri kila litokapo kabla sijalipandisha kwenye tovuti ya Times FM, miaka mitano iliyopita.

Nikki alionesha uwezo mkubwa wa kifikra na kupanga hoja, yuko ‘very smart’. Kwa lugha fupi ya mtaani ‘anajua’.

Utamuona pia kwenye utetezi wa sanaa ya Tanzania.

Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete (kushoto) akikabidhiwa picha maalum yenye majina ya wasanii karibu wote, kutoka kwa Msanii Nickson ‘Nikki wa PIli’ Simon

Hata hivyo, Ndoto ya Nikki, wengi waliichukulia kama ndoto ya al-Nacha. Nikupe kidogo kuhusu Al-Nacha, kijana ambaye wengi huwa hatujui kisa chake.

Kwa kifupi, Al-Nacha alikuwa kijana maskini aliyekuwa na mtaji wa reale 100 tu alizopewa kama urithi, akaziweka zote kwenye mtaji wa vyombo vya udongo (glass). Kisha akaanza kuota kuwa atauza vyombo hivyo na kuwa na utajiri wa kufanya biashara ya almasi, kumiliki watumwa, kumuoa binti mzuri wa waziri na kuishi maisha ya kifalme. Lakini wakati anaendelea kuota ubwanyenye alijikuta akipiga teke kapu lenye vyombo hivyo na kila kilicho ndani kikavunjika, akarejea kwenye umasiki wa kutupwa zaidi ya awali.

Nimeamua kuimulika ndoto hii ya Nikki wa Pili, kijana msomi mwenye Shahada ya Uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mwenye uwezo mkubwa wa kujenga hoja na kutetea kile anachokiamini.

Kwa haraka-haraka, nikaona kuna pande mbili za ndoto hii. Kuzipitia pande hizo, unapaswa kujibu ni kwanini inawezekana na kwanini haiwezekani.

A: Kwanini inawezekana?

  1. Katiba sio msaafu

Katika kufuatilia, wengi walikuwa wanasema kuwa Nikki wa Pili haonekani kuwa kada wa chama chochote hivi sasa hivyo hawamuoni Nikki akipenya kwenye kuta hizo. Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, mgombea lazima apitishwe na chama chake ili apewe baraka za kuwania nafasi ya urais, kitu ambacho Nikki haonekani kukifanikisha hivi karibuni.

Lakini tukumbuke kuwa kwenye siasa, kila dakika moja inaweza kuleta mabadiliko makubwa. Nani angejua kuwa leo kuweka habari za video kwenye mtandao unapaswa kuwa umesajiliwa na kulipia? Kama ilivyo kwa sheria, Katiba ya nchi inaweza kubadilika kwa matakwa na mahitaji ya wakati husika ingawa mchakato wake ni mzito kidogo kuliko wa sheria. Huenda siku moja… huenda hata mwakani tu, katiba ikaruhusu ‘mgombea binafsi’.

Hapo Nikki anaweza kuwa ameruka kiunzi cha kutokuwa na chama, umri ukiwa unaruhusu atagombea kama mtanzania yeyote mwenye haki na fursa hiyo. Suala kushinda au kushindwa ni uamuzi wa wapiga kura.

  1. Hakuna kituo cha kuanzia siasa

Wengi wamehoji uzoefu wa Nikki kwenye mkondo wa siasa. Kwamba hajawahi kuonekana kwenye ulingo wa siasa na hajawahi kuonekana kujihusisha. Ni kweli, Nikki hata kwenye nyimbo zake anaweza kuwa ni mtu wa kuelimisha zaidi, na sio mtu anayeonekana kama ana mlengo wa kuwa kiongozi hata ngazi ya udiwani!

Lakini huwezi jua. Nitakupa mfano wa jinsi ambavyo siasa haitabiriki. Nani angedhani leo Jerry Muro, mtangazaji aliyejipatia heshima kupitia kipindi cha kufichua ulaji rushwa na kuwaonesha watanzania kwenye runinga. Baadaye kuwa msemaji wa klabu ya Yanga, ndani ya muda mfupi alibadilika na kutangaza nia ya kugombea ubunge Kinondoni, ndoto hiyo ilipoonekana kuyeyuka mengi yakaendelea chini ya kapeti leo ni Mkuu wa Wilaya na inadaiwa huenda akawania Ubunge miaka miwili ijayo, hatujui nini kitafuata. Ni mfano tu wa kumpa moyo Nikki.

Wengi wametumia mifano ya maisha ya siasa ya Dkt. Jakaya Kikwete, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na hata Rais John Magufuli kuipiga teke ndoto ya Nikki. “Urais ni mfumo,” nimesikia kwenye mjadala wa SnS. Kweli hoja nzito hii.

Lakini tujaribu kufikiria, wangapi tulikuwa tunamfahamu Hashimu Rungwe kabla ya kugombea urais? Nani anajua kuwa hataweza kabisa kuwa Rais siku za usoni? Anajua mwenyewe alipoanzia. Kwa mfano!

Nikki wa Pili aliwahi kurap kwenye Niaje Ni Vipi, “Ni vipi Bro unatabiri hawatanipenda, hakuna aijuae kesho hata mtunzi wa kalenda.”

  1. Kwa Chadema anaweza kulianzisha paaaap!

Tofauti na ilivyo kwa katiba ya CCM na sifa za kuwania nafasi ya Urais, kwa mujibu wa Katiba ya Chadema mtu anayejiunga na chama leo ana sifa na haki kama mwanachama yeyote bila kujali uzoefu. Je, Nikki akiamua kuwania kuanzia kura za maoni huko baada ya kujiunga muda huo, si anaweza kuingia kwenye kinyang’anyiro na ikawa hatua ya kwanza? Japo maandishi nayo sio vitendo, wakati mwingine!

  1. Sio mwanamuziki wa kwanza kuota urais na kuwa rais

Nikki wa Pili anaweza kuwa anaota lakini isiwe ndoto yake peke yake, iliwahi kuotwa na wanamuziki wengine. Kaka yake, Joh Makini aliwahi kurap, “Ndoto ni kuamka kuikimbilia.”

Nikupe mfano wa marais wa Marekani ambao waliwahi kuwa wanamuziki kabla, tena hata hawakujulikana sana, baadaye waliamua kuwa wanasiasa na wakawa marais wengine bila hata kutarajiwa mapema. Mfano, Thomas Jefferson (1801 –1809), John Quincy Adams (1825 –1829), John Tyler (1841 – 1845), Warren G. Harding (1921 – August 2, 1923), Harry Truman (1945 –1953), Richard Nixon (1969 –1974).

Mfano Harry Truman, Rais wa 33 wa Marekani, yeye alikuwa anashindwa kujizuia hata alipokuwa ikulu, akicheza piano kwa namna yake. Tangu akiwa mdogo alikuwa na ndoto ya kuwa mwanamuziki, akawa mwanaumizi. Lakini baadaye aliongeza ndoto ya kuwa mwanasiasa, akaamka akaikimbilia na ‘ikatiki’, japo haikuwa rahisi.

Rais wa 33 wa Marekani, Harry Truman 

Kwa Tanzania wanamuziki waliowahi kutangaza kuota urais pia ni pamoja na Kala Jeremia. Ingawa Roma Mkatoliki hajawahi kusema wazi, wengi wanaamini ile 2030 ndiyo ndoto yake ya kugombea urais!

 B: Kwanini Nikki ana ndoto ya Al-Nacha?

  1. Nikki ana upungufu wa sifa hii muhimu 

Pamoja na mambo mengine, historia fupi ya maisha ya Nikki na jinsi nilivyowahi kukutana naye au kumsikia akizungumza, kufanya naye mahojiano mara zaidi ya tano nazokumbuka, nilibaini kuwa Nikki anaupungufu wa vitamini za uvumilivu.

Nikiachana na fikra zangu tu, ambazo huenda zisiwe sahihi pia… huenda siku hizo alikuwa na ‘mood’ tofauti… naweza kutumia mfano mwingine, kwa namna ambavyo nimekuwa namsikiliza akipambana na mawazo kinzani, hivi karibuni alionesha upungufu wa uvumilivu aliposhambuliwa kwenye mitandao ya kijamii hasa na Mange Kimambi. Nikki alishindwa kuvumilia maneno tu na kutangaza kuachana kabisa na masuala ya siasa!! Anakata tamaa! 

Waingereza wanasema kanuni muhimu ni ‘Don’t Quit, Don’t give up’.

Anasahau moja kati ya sifa kuu ya kuwa mwanasiasa ni kama kuwa bondia, uwe na uwezo wa kuvumilia masumbwi tena ya uso. Ulingo wa siasa sio sehemu laini ya mterezo, amuulize vizuri Mheshimiwa Edward Lowassa mwenye ndoto kama yake. Uvumilivu na busara ndivyo vilivyompa tuzo kubwa Afrika mwaka 2016 baada ya kukosa urais 2015.

  1. Ana ndoto ya ubondia kwa mazoezi ya tenesi

Nadhani Nikki wa Pili kwa sasa ni kama mtu ambaye ana ndoto ya kuwa bondia bingwa kama Floyd Mayweather na Manny Pacquiao lakini bado amejikita kwenye mazoezi ya mchezo mwingine kabisa, mfano wa tenesi.

Hii ndiyo pointi ya wengi wanaompinga Nikki na ndoto yake. Hajaonesha nia kweli ya kuwa kwenye ulingo sahihi na kufanya kile kinachotakiwa kufanywa na mtu ambaye anataka kushika nafasi ya juu zaidi ya uongozi nchini. Yaani ni kama anategemea kuangukiwa na dafu akiwa chini ya muembe.

  1. Urais ni taasisi, mfumo 

Urais ni taasisi ambayo inajengwa na mfumo. Hivyo, kila ambaye anatakiwa kuwa Rais, hasa kwenye nchi kama Tanzania ni lazima aingie kwenye mfumo. Hilo halina pingamizi. Nikki anapaswa kuanza kuwa ndege anayeruka na kundi la ndege walio kwenye njia sahihi ya mfumo. Aaanze kutengeneza CV yake kwenye nyanja hizo, la sivyo hataweza.

Hata kwenye vitabu vya Mungu, kila kiongozi wa ngazi za juu hakutokea hewani. Mungu alimuandaa na akaona utayari wake. Kuna CV kama ya Mfalme Daudi, yeye aliandaliwa kuanzia nyikani alikokuwa anachunga na yeye alijinoa kuwa mpambanaji kweli bila kukata tamaa, wakati huo CV kubwa ilikuwa ni lazima uwe shujaa ndipo uwe mfalme. Pia, alipata nafasi ya kukaa pembeni ya Mfalme (japo alikuwa adui kwake) na hapo akajifunza ‘siasa’ ya utawala.

Nikki anahitaji kutengeneza CV husika mapema.

Mwisho, sina haja ya kumkatisha tamaa kwenye ndoto yake. Aliyebuni Kompyuta ninayotumia kuandikia haya pia ndoto yake ilikuwa ya ajabu wakati  huo na naamini haikuwa inaleta maana. Leo imekuwa kweli.

Narudia, “Hakuna aijuaye kesho hata mtunzi wa kalenda.” Lakini pia, “huwezi kuwa bondia bingwa kwa mazoezi ya tenesi.”

Video: Ridhiwani achangia milioni 5 ujenzi wa ofisi za CCM Kata ya Kiwangwa
Bobi Wine aachiwa, akamatwa tena na Jeshi la Polisi