Spika wa Bunge Job Ndugai amesema baadhi ya Wabunge wamekuwa wakipiga makofi bungeni lakini haijulikani wamepiga ya nini.

Ndugai amesema hayo jana wakati Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Khamis Hamza Khamis akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa viti maalumu (CCM) Husna Sekiboko kwamba polisi wamekuwa wakishindwa kufika kwa wakati maeneo mbalimbali kwa sababu ya kukosa mafuta na matengenezo ya magari.

Awali, akijibu swali Khamis alisema kwa mujibu wa sheria ya bajeti wenye fungu ni Mkuu wa Polisi nchini (IGP) na Ma-RPC hivyo fungu likitoka kwa IGP linakwenda kwa RPC na kisha kugawiwa kwa Wakuu wa Polisi wa Wilaya husika na kuongeza kuwa  wanalichukua suala hilo na kwenda kukaa na wadau ili kuona namna wanavyoweza kulifanyia mabadiliko.

Hata hivyo, majibu hayo yaliwafanya baadhi ya wabunge kumpigia makofi Naibu Waziri huyo, hali iliyomuibua  Ndugai ambaye alisema kuna wakati Wabunge wanapiga makofi haifahamiki wanapiga ya nini.

Ndugai alihoji, “Halafu waziri akakae na wadau, wakina nani? Halafu tunashangilia (wabunge) tunakubali hiyo kanzu.”

Marekani kurejea Baraza la Haki za Binadamu
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Februari 9, 2021