Serikali ya Malawi inadaiwa kufungua tena ukurasa wa mgogoro kati yake na Tanzania kuhusu umiliki wa Ziwa Nyasa inalodai ni Ziwa Malawi.

Hayo yamebainika kupitia barua ya Katibu Mkuu Kiongozi wa Malawi, George Mkondiwa iliyotajwa kuwa na Kumbukumbu No. CS/S/001 ikienda kwa makatibu wakuu na ngazi nyingine za chini ikieleza msimamo wa nchi hiyo kuhusu umiliki wa Ziwa Nyasa liliko katika mpaka wa Tanzania na nchi hiyo.

Kwa mujibu wa Mtanzania, barua hiyo iliyokuwa na kichwa cha habari ‘Malawi and Tanzania Dispute over Lake Malawi Boundary’ (Mgogoro wa Malawi na Tanzania kuhusu mpaka wa ziwa Malawi {Ziwa Nyasa}), imewaeleza makatibu wakuu hao kuwa Serikali ya Tanzania imekuwa ikitumia vyombo vya habari kutoa ramani inayoonesha ziwa hilo liko Tanzania.

“Kutokana na mwenendo wa propaganda zinazofanywa na Serikali ya Tanzania kupitia vyombo vya habari, Serikali ya Malawi inatoa msimamo wake kwamba mipaka yake haitabadilika na daima itabaki kama ilivyowekwa katika Mkataba wa Anglo Heligoland,” sehemu ya barua hiyo imekaririwa.

Kwa upande wa Tanzania kupitia Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustino Mahiga amesema kuwa bado hajaiona barua hiyo na kwamba anachofahamu suala hilo bado liko kwenye Kamati ya Usuluhishi iliyoundwa.

“Jambo hili linafanyiwa usuluhishi na marais wawili wa zamani wa Afrika Kusini na wa Msumbiji, na usuluhishi bado unaendelea. Tunasubiri ripoti ya usuluhishi,” Balozi Mahiga anakaririwa.

Balozi Mahiga aliongeza kuwa upande mmoja hauwezi kutolea msimamo mgogoro huo kwani bado uko kwenye hatua za usuluhishi.

Hii ni mara ya kwanza Malawi kufufua mgogoro huu tangu Rais John Magufuli aingie madarakani Novemba 5 mwaka jana.

Malawi imekuwa ikidai Ziwa Nyasa liko upande wake na imelipa jina la Ziwa Malawi na kulijumuisha kwenye ramani yake.

Chidi Benzi Arudi Tena Kwenye Madawa Ya Kulevya
Chukua hii: Lipumba alitaka Jaji Warioba agombee Urais kupitia Ukawa, Sio Lowassa