Mkuu wa Idara Ya Habari Na Mawasiliano ya klabu ya Ruvu Shooting Masau Bwire, ametoa maoni kuhusu maamuzi ya michezo iliyosalia ya ligi kuu kuchezwa katika kituo cha Dar es salaam.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Harrison Mwakyembe juma lililopita alitangaza viwanja vya Uhuru, Taifa na Azam Complex vyote vya Dar es salaam, kutumika kwa michezo ya ligi kuu iliyosalia msimu huu 2019/20.

Waziri Mwakyembe alisema maamuzi ya michezo ya ligi kuu kucheza katika kituo cha Dar es salam, yametokana na uhaba wa kiuchumi ambao umeziandama klabu nyingi, kufuatia janga la maambukizi ya Corona ambalo lilipelekea shughuli nyingi kiuchumi kusimama.

Msau amesema maamuzi ya ligi kuchezwa Dar es salaam, huenda yakawa mzigo mkubwa kwa klabu kadhaa za ligi hiyo, kutokana na jiji hilo kuwa na gharama kubwa za kimaisha.

Masau amesema kwa siku 36 ambazo zinakadiriwa huenda ligi ikachezwa jijini Dar es salaam, huenda kila timu shirikia ikatumia zaidi ya shilingi milioni 50.

“Ukipiga hesabu kwa wachezaji, benchi la ufundi na uongozi kila timu itakuwa na watu 30 kambini Dar es salaam na watakaa zaidi ya siku 36, gharama za hoteli kwa mtu mmoja kwa siku ni shilingi 40,000 zidisha kwa watu 30, kisha zidisha kwa siku 36 unapata zaidi ya shilingi Mil. 43”

“Chakula kwa mtu mmoja kwa siku kiwango cha chini ni 15,000 zidisha kwa watu 30 na uzidishe kwa siku 36 unapata zaidi ya Tsh. Mil. 16”

“Hapo tu utahitaji kuwa na zaidi ya tsh. Mil. 59. Kuna gharama za mazoezi ambazo zinaweza kupanda kutoka laki 1 hadi 2 kwa siku kisha zidisha kwa siku 20 za mazoezi, kuna gharama za usafiri na mambo mengine tofauti na kusafiri mechi 4 au 5 za ugenini.

Kwa hiyo ligi kuchezwa Dar es salaam pekee ni mzigo mkubwa ambao vilabu vingi vitashindwa kuubeba”

Wakati ligi kuu ikitarajiwa kuendelea katika kituo cha jijini Dar es salaam, ligi daraja la kwanza na ligi daraja la pili zimepelekwa jijini Mwanza katika viwanja vya CCM Kirumba na Nyamagana.

Morogoro: Mchungaji afanya maombi kwa kuwaingilia kimwili waumini, mwanafunzi apata mimba
Mkwasa: Wachezaji wamepoteza uwezo wa kumiliki mpira