Meneja wa klabu bingwa nchini Italia Juventus FC, Massimiliano Allegri amepinga mpango wa kiungo kutoka Ufaransa, Paul Pogba wa kupigiwa chepuo la kurejea Man Utd katika kipindi hiki cha usajili.

Allegri, alisema hakubaliani na mpango huo kutokana na kuamini kwamba, kama itatokea Pogba anakubali kurejea Old Trafford itakua sawa na mtu kukubali kurejea nyuma katika safari ya kusaka mafanikio maishani mwake.

Pogba amekua akihusishwa na taarifa za kuondoka Juvetus Stadium, tangu mwishoni mwa msimu uliopita, na majuma mawili yaliyopita uongozi wa klabu hiyo ya mjini Turin ulitangaza kiasi cha Pauni milion 100 kuwa ada yake sahihi kwa yoyote atakayejitokeza na kutaka kumsajili.

Meneja huyo kutoka nchini Italia, alisema kwa sasa ni wakati mzuri kwa Pogba kuamini kuna nafasi kubwa ya kuangalia mbele na si kutazama alipotoka ambapo alijaribu bahati yake na ilionekana hapewa thamani.

“Sishangazwi na tetesi za Pogba kutakiwa na Man Utd,” Allegri alikaririwa na gazeti la michezo la nchini Italia (Gazzetta dello Sport).

“Kila mmoja ana bahati yake katika maisha na mchezaji huyo kuondoka Juventus ni jambo la kawaida, lakini tunapwaswa kumshauri kwa kumuelekeza ni wapi anapaswa kwenda kuendeleza uwezo wake.

“Hii sio klabu ambayo inakubali kumuuza mchezaji kinyemela, bali tunaangalia ni wapi anapoelekea. Pogba bado ni mali ya Juventus mpaka siku atakayoamuriwa kundoka, hivyo tunapaswa kumsaidia kwa kila hali.

Allegri anaamini Juventus ni moja ya klabu kubwa barani Ulaya na inajivunia kuwa na mchezaji kama Pogba mwenye umri wa miaka 23, ambaye alisajiliwa kama mchezaji huru akitokea Man Utd mwaka 2012.

Alisema kwa kiwango walichonacho Juventus kwa sasa daima hakiwezi kushabihiana na Man Utd, tena akatumia mfano wa michuano watakayoshiriki msimu ujao barani Ulaya, ambapo mabingwa hao wa Italia watacheza ligi ya mabingwa barani humo na mashetani wekundu watapambana kwenye mshike mshike wa Europa League.

Pogba, alikua sehemu ya kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa ambacho kilifika kwenye hatua ya fainali ya michuano ya Euro 2016 na alionyesha kuwa muhimili mkubwa kwenye mafanikio yaliyopatikana kabla ya kupoteza mchezo wao wa mwisho dhidi ya Ureno.

Kiungo huyo pia alisaidia kuifikisha Juventus katika mchezo wa fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya mwaka 2015, lakini kwa bahati mbaya walipoteza kwa kufungwa na FC Barcelona mabao matatu kwa moja.

Leicester City Kumuweka Sokoni Riyad Mahrez
Serikali Imekitoza Faini Kiwanda cha Sabuni (Royal Soap industry).