Sekta za mazingira na Maliasili kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zimekubaliana uhifadhi endelevu, usimamzi wa mazingira na maliasili zilizopo katika ukanda huu.

Naibu Waziri ofisi ya makamu wa Rais Khamis H. Khamis ameyasema hayo baada ya kushiriki mkutano wa 8 wa baraza la kisekta la Mawaziri wa mazingira na maliasili wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika mwishoni mwa wiki jijini Arusha.

Amesema pamoja na makubaliano hayo pia wamepata fursa ya kujadili na kuwekeana mikakati ya uhifadhi wa mazingira itakayowashirikisha wananchi ambao ni sehemu ya sulihisho.

“Tumejadiliana na kukubaliana kuelimisha wananchi kuhusu matumizi bora ya ardhi tunaona migogoro mingi ya ardhi kwasasa na watu wanafanya uharibu wa mazingira kupitia ardhi,” amesema Naibu waziri Khamis.

Awali Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja amesema mkutano huo umewapa fursa ya kujadili mikakati ya usimamizi wa mazingira na maliasili katika ukanda wa Afrika Mashariki.

“tumepata fursa ya kujadili mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi zinazoathiri maendeleo ya kijamii miongoni mwa wananchi wetu,” amefafanua Naibu Waziri Bi. Mary

Kwa upande wa kiongozi wa mkutano huo na Waziri wa Mazingira na Maliasili wa Kenya Keriako Tobiko amesema changamoto ya uharibifu wa mazingira bado inaukabili ukanda wa Afrika Mashariki na hivyo kuhatarisha maisha ya raia.

Amesema hali hiyo inatoa jukumu kwa nchi wanachama kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha changamoto za uharibifu wa mazingira zinafanyiwa kazi kwa mafanikio.

Naye Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Peter Mathuki amesema baada ya kuhitimishwa kwa mkutano huo nchi wanachama wamepanga na wanatarajia kutekeleza makubaliano yote.

“Katika changamoto hii ya mabadiliko ya tabia nchi mawaziri wana wajibu wa kuhakikisha wananchi wanapata manufaa ya kile tulichokubaliana kuhusu uhifadhi wa mazingira,” amefafanua Mathuki.

Mkutano huo umeshirikika nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki zikiwemo Tanzania, Uganda, Kenya, Sudan Kusini, Burundi na Rwanda.

Zelensky: Diplomasia ndiyo itamaliza vita
Habari Kuu katika magazeti ya leo Mei 22, 2022