Uongozi wa Mbao FC umebaini utovu wa nidhamu ulikithiri katika kikosi chao wakati wa mchezo dhidi ya Simba uliochezwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza mwanzoni mwa juma hili.

Mbao FC walipoteza mchezo wao dhidi ya Simba mwanzoni mwa juma hili kwa kufungwa mabao matatu kwa mawili, hali ambayo ilizua mshangao kwa mashabiki wa soka nchini. Mbao FC walikua wakiongoza mabao mawili kwa sifuri hadi katika dakika ya 82, lakini Simba walitumia muda uliobaki kusawazisha na kuongeza bao la ushindi.

Afisa habari wa Mbao FC, Crinstant Malinzi amesema uongozi wa ngazi ya juu wa klabu hiyo walikutana kwa dharura na kubaini dalili za udanganyifu uliofanywa na mlinda mlango Erick Ngwengwe.

Akizungumza na Dar24, Malinzi amesema uchunguzi wa kina unaendelea kufanywa dhidi ya mlinda mlango huyo sambamba na wachezaji wengine ambao wanahisiwa kushiriki kwenye udanganyifu ambao unadaiwa kuchagiza ushindi wa Simba.

“Tumemsimamisha kipa wetu ili kupisha uchunguzi ili kubaini kama kweli alihusika na udanganyifu wa kufungisha kwa makusudi, tumekubaliana hatoshiriki hata katika mazoezi ya timu katika kipindi hiki ambacho anafanyiwa uchunguzi.

“Uchunguzi huu utawahusisha wachezaji wengine ambao tunahisi walihusika kwa namna moja ama nyingine, lengo letu ni kutaka kuiwezesha Mbao FC kubaki salama ili ifanikishe mpango wa kupambana, na kusalia katika ligi kuu msimu ujao.” Amesema Malinzi.

Kufungwa kwa Mbao FC katika mchezo dhidi ya Simba kumeendelea kuiweka pabaya klabu hiyo ya jijini Mwanza kwenye msimamo wa ligi kuu ya soka Tanzania bara, na kama itahitaji kujinusuru na janga la kushuka daraja italazimika ishinde michezo yote iliyosalia.

Mwishoni mwa juma hili Mbao FC watacheza mchezo mwingine katika uwanja wa CCM Kirumba dhidi ya Tanzania Prisons kutoka jijini Mbeya.

Michezo mingine itakayoikabili Mbao FC kuelekea mwishoni mwa msimu huu ni dhidi ya Azam FC (Azam Complex), Kagera Sugar (Uwanja wa Kaitaba) na Young Africans (Uwanja wa Taifa).

Mbao FC wapo kwenye nafasi ya 13 kwa kufikisha point 27, ikiwa ni tofauti ya point tatu dhidi ya Toto Africans wanaoburuza mkia kwa kumiliki point 23.

Tuzo Za PFA: Harry Kane, Romelu Lukaku Kuumana Tuzo Mbili Tofauti
Live: Kongamano la Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere