Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amelalamikia hatua ya jeshi la polisi kupitia ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) kumuita kwa ajili ya mahojiano mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho, Edward Lowassa na kisha kuahirisha na kutoa tarehe nyingine.

Mbowe ametumia mtandao wa Twitter kueleza malalamiko yake, akidai kuwa kitendo hicho ni ubabe na usumbufu, kwani kulikuwa na uwezo wa kumpa taarifa hata kabla hajaenda kituoni hapo.

Katika hatua nyingine, Mbowe amekosoa hatua ya jeshi la polisi kuwafukuza waandishi wa habari waliofika katika eneo hilo kwa lengo la kuchukua habari akidai walikuwa na haki ya kupata habari ya tukio hilo.

“Huu ni kama usumbufu na ubabe kwa namna moja au nyingine, walikuwa na uwezo wa kutoa taarifa kwa Mhe. @edwardlowassatz asiende leo,” inasomeka tweet ya Mbowe.

“Waandishi wa Habari wanafukuzwa, unapomuita Kiongozi wa kisiasa kama Mhe. @edwardlowassatz ni habari wanayo haki ya kujua kinachoendelea,” aliongeza kwenye tweet nyingine.

Lowassa aliitwa na kuhojiwa na DCI hivi karibuni kwa kauli yake aliyoitoa wakati wa kushiriki futari iliyoandaliwa na madiwani wa Chadema, ambapo alimuomba Rais Magufuli kuwaachia huru mashehe wa Jumuiya ya Uamsho, na kuamriwa kurejea leo kwa ajili ya mahojiano zaidi.

Leo, Lowassa akiwa ameongozana na baadhi ya viongozi wa chama hicho walifika katika Makao Makuu ya Polisi, lakini mahojiano hayo yameahirishwa na anatakiwa kurejea Julai 13 mwaka huu.

Video: CCM waunga mkono kauli ya JPM
Kaimu Jaji Mkuu awapa neno mawakili, ataka haki itendeke katika jamii