Mbunge wa jimbo la Ulanga, Goodluck Mlinga (CCM) aliyepata umaarufu zaidi kwa kupendekeza bungeni kutengenezwa kwa sanamu ya Diamond Platinumz, jana aliibuka na mashtaka ya aina yake dhidi ya mbunge wa Chadema, Anatropia Theonest.

Mbunge huyo amefikisha mashtaka yake kwa Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson akidai kuwa mbunge huyo wa Chadema alimvua kofia inayovaliwa na kanzu (bagalashee) na kutokomea kusikojulikana kabla ya kuanza kwa vikao vya Bunge.

Alisema kutokana na taratibu za Bunge kuwa wanaovaa Kanzu lazima waingie Bungeni wakiwa na kofia hiyo, alishindwa kuhudhuria kikao kwa muda hadi alipopewa kingine na mbunge aliyemuita ‘msamalia mwema’.

“Wakati waheshimiwa wabunge wa upinzani wanatoka nje, kundi la wabunge wa Chadema likiongozwa na mbunge Anatropia Theonest lilifika lilifika kwenye meza yangu na alinivua kofia yangu kama hii (alionesha kofia aliyovaa). Hii nimepewa na msamalia mwema hapo nje ili niweze kudhuria kikao cha Bunge,” alisema Mlinga.

Mbunge huyo alieleza kuwa kitendo hicho kimemuachia mtikisiko wa mawazo kwakuwa hafahamu nia yam bunge huyo, huku akieleza athari alizosababishiwa ikiwa ni pamoja na kutowatendea haki wapiga kura wake kwa kutoingia Bungeni kwa muda.

Kadhalika, alisema kuwa Mbunge huyo amemkosea mkewe kwa kuingia kwenye himaya yake na kukosea amri ya tisa ya Mungu inayowataka wasitamani mali ya mtu mwingine, kwani ‘amemtamani mwanamume wa mtu mwingine”.

Baada ya kusikiliza mashtaka ya Mlinga, Naibu Spika alisema kuwa hajapewa taarifa ya tukio hilo na kwakuwa hakulishuhudia hawezi kulitolea maamuzi. Alielekeza Kamera za Bunge kusaidia kuwasilisha ushahidi wa malalamiko hayo.

Wabunge wa Upinzani wameendelea kutekeleza azimio lao la kutoshirikiana na wabunge wa CCM hata kwa kusalimiana nao huku wakiendelea kususia vikao vya Bunge. Wabunge hao wanadai kukandamizwa na Naibu Spika wakidai kuwa anaendesha Bunge kwa upendeleo, kuilinda Serikali, kuwakandamiza wapinzani na kuvunja kanuni za Bunge.

Mtoto wa Michael Jackson afunguka baada ya picha ‘chafu za watoto’ kukutwa chumbani kwa Michael
Sitaki Nataka Za Slaven Bilic Kwa Alexandre Lacazette