Rufaa ya mshambuliaji na nahodha wa FC Barcelona Lionel Messi ya kupinga adhabu ya kadi ya njano aliyooneshwa wakati akishangulia bao kwa kutoa heshima kwa gwiji wa soka duniani Diego Maradona, imegonga mwamba.

Messi alishangilia kwa ishara ya kutoa heshima ya kipekee wakati alipofunga bao kwenye mchezo wa Ligi ya Hispania dhidi ya Osasuna, huku picha ya tukio hilo ikigonga vichwa vya habari duniani.

Akiwa anashangilia, nahodha huyo wa timu ya taifa ya Argentina alivua jezi yake ya Juu, na kubaki na jezi aliokua ameivaa ndani iliyokua na namba 10, ambayo ilikua ikitumiwa na Diego Maradona ambaye aliyefariki dunia mwishoni mwa mwaka jana.

Mwamuzi wa mchezo huo Mateu Lahoz alimuonesha kadi ya njano Messi, hatua ambayo ilipelekea Shirikisho la soka nchini Hispania kutangaza adhabu kwa FC Barcelona na mshambuliaji huyo kulipa Euro 3000.

Kwa maamuzi hayo ya adhabu FC Barcelona walikata rufaa ya kutaka kufutwa kwa adhabu hiyo, lakini mambo yalikua magumu licha ya kupunguzwa kwa faini na kufikia €600, kwa mujibu wa kifungu cha 91 cha Kanuni za Nidhamu za Shirikisho la Soka Hispania.

Hata hivyo FC Barcelona bado wanaweza kukata rufaa kwenye Mahakama ya Usuluhishi ya Michezo (CAS), lakini bado hakuna dalili kama watachukua uamuzi huu.

Kisheria FC Barcelona wana muda wa siku 15 za kukata rufaa CAS, baada ya maamuzi ya rufaa ya awali kutangazwa na Shirikisho la soka nchini Hispania.

Bob wine apinga matokeo
Tetesi za usajili: Ighalo kutimkia Marekani