Afisa kutoka Ofisi za Mkemia Mkuu wa Serikali, Elias mulima jana alitoa ushahidi wake mahakamani kuhusu mkojo wa Agnes ‘Masogange’ Gerald akidai kuwa ulikuwa na dawa za kulevya aina ya Heroine, ikiwa ni saa takribani sabini baada ya kuiambia Mahakama hiyo kuwa walikuta bangi kwenye mkojo wa Wema Sepetu.

Mulima aliiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana kuwa Februari 15 mwaka huu kwa kufuata utaratibu wa kisheria walichukua sampuli ya mkojo wa Agnes na kuifanyia vipimo katika  maabara.

Shahidi huyo aliieleza Mahakama kuwa matokeo ya vipimo hivyo yalibaini kuwepo chembechembe za Heroine na Oxazepam ambayo yote ni aina ya madawa ya kulevya.

Alisema kuwa baada ya kukamilisha uchunguzi huo, Ofisi ya Mkemia Mkuu iliandaa taarifa maalum ambayo Agnes aliisaini na baadae kuthibitishwa na Mkemia Mkuu.

Hata hivyo, mawakili wa Agnes, Nehemiah Nkoko na Reuben Simwanza walimtetea mteja wao wakiiomba Mahakama kutopokea fomu za matokeo ya vipimo hivyo kwa madai kuwa utaratibu wa kisheria haukufuatwa.

Wakili Nkoko alisema kuwa sheria inataka kabla ya kuchukua sampuli ya mkojo wa mtuhumiwa, polisi waombe kibali mahakamani kitu ambacho alidai hawakufanya. Hivyo, aliiomba mahakama isivipokee vielelezo hivyo kwani viko kinyume cha sheria.

Utetezi huo ulifanana na ule alioutoa Wakili wa muigizaji Wema Sepetu, Peter Kibatala wiki hii katika mahakama hiyohiyo baada ya Mulima kutoa ushahidi kuwa vipimo vya sampuli ya mkojo wa msanii huyo vilikutwa na bangi.

Aidha, Wakili wa Serikali, Constatine Kalula alipinga utetezi wa wakili wa Masogange kwa sababu kama zilizotolewa wakati wa kupinga utetezi uliotolewa Kibatala.

Kakula alisema kuwa kwa mujibu wa sheria sio lazima kuomba kibali mahakamani ili kuchukua sampuli ya mtuhumiwa isipokuwa pale ambapo mtuhumiwa huyo amekataa kuchukuliwa vipimo na kwamba hakuna sehemu ambayo wameeleza kuwa alikataa. Hivyo, aliiomba mahakama kutupilia mbali pingamizi la kupokea vipimo hivyo lililowekwa na upande wa utetezi.

Baada ya mvutano huo wa kisheria, Hakimu aliahirisha shauri hilo hadi Agosti 28 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena ambapo uamuzi kuhusu kupokea au kutopokea sampuli hiyo utatolewa.

Agnes yuko nje kwa dhamana akitakiwa kutotoka nje ya mkoa wa Dar es Salaam bila kibali maalum cha Mahakama.

RC Makonda kubadili mfumo wa utendaji kazi wa Polisi Dar
Video: Rais Magufuli akiwasili Tanga, kuelekea uzinduzi wa bomba la mafuta