Watumishi wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili na uwajibikaji ili kutenda haki kwa kila mwombaji wa ajira serikalini ambaye ana sifa za kupata kazi kwa mujibu wa nafasi husika zinazotangazwa na Taasisi mbalimbali za umma.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst) George Mkuchika (Mb) wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kilichofanyika mjini Morogoro.

Mkuchika amewasisitiza watumishi hao kuendelea kuzingatia Uadilifu, Sheria, Kanuni na Taratibu zinazosimamia Utumishi wa Umma nchini kwani kazi wanayoifanya ni nyeti na inagusa maisha ya watu, hivyo inahitaji watu waadilifu, wapenda haki na ambao ni mfano wa kuigwa na jamii kwa uadilifu.

Aidha, Mkuchika amesema, ni muhimu watumishi wa Sekretarieti ya Ajira kuwahudumia wateja wao kwa lugha nzuri kwani ndio nyenzo muhimu katika utoaji wa ajira.

“Tumieni lugha nzuri na zenye staha kwa kuwasikiliza na kuwahudumia vizuri wateja wenu kwani nyie ndio lango kuu la kuingiza watu katika Utumishi wa Umma, hivyo mienendo yenu ndio picha ya aina ya watumishi watakaopatikana kwa ajili ya kuja kusimamia utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo inayofanywa na Serikali”, amefafanua Mkuchika.

Mkuchika amewahimiza watumishi hao, kufanya kazi kwa kushirikiana na waajiri kwani jukumu walilopewa la kuendesha mchakato wa ajira ni kwa niaba ya waajiri hivyo ni muhimu wakashirikiana kuhakikisha mchakato huo unakwenda vizuri na kwa wakati.

'Naomba CAG aje haraka ili niwe huru na Ubunge wangu' - Tabasamu
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Desemba 23, 2020