Mnada wa pili wa makontena 20 yenye samani zikiwamo meza na viti, yaliyoingizwa nchini na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, utafanyika Septemba Mosi baada ya ule wa Agosti 25 kutofanikiwa kupata wanunuzi.

Makontena hayo ambayo yamekwama bandarini yanadaiwa kodi ya Sh bilioni 1.2.

Hayo yamesemwa jijini Dar es salaam na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa (TRA), Richard Kayombo, ambapo amesema kuwa mamlaka hiyo imeazimia kufanya mnada wa pili Jumamosi.

“Tunatarajia kufanya mnada wa pili wa makontena 20 yaliyopo kwenye bandari kavu ya Dar es Salaam ifikapo Septemba mosi mwaka huu (Jumamosi),”amesema Kayombo.

Aidha, amesema kuwa mnada huo utaanza saa 2:00 asubuhi kwa kufuata taratibu zote za sheria kama mnada wa awali ulivyofanyika, hivyo wananchi wanapaswa kujitokeza kwa ajili ya kununua samani hizo kwa kufuata taratibu na sheria za minada.

Hata hivyo, ameongeza kuwa TRA haiwezi kutangaza bei ya mnada huo kabla ya kufanyika kwa sababu ni siri, lakini wateja watakaofika watakuta bei ambayo imepangwa kwa mujibu wa sheria ili serikali iweze kupata mapato yake.

 

DC Kasesela atembelea kijiji ambacho hakijatembelewa na DC tangu 2010
Video: Lowassa ashtuka, Tamko la Serikali mwanafunzi aliyeuawa Bukoba