Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella amewaagiza viongozi wa Wilaya na Halmashauri Karatu kusimamia miradi ya maendeleo ili iweze kukamilika kwa wakati na wananchi waanze kupata huduma.

Mongella ametoa agizo hilo alipofanya ziara ya siku moja ya kukagua miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Karatu na kueleza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kwa wakati kutasaidia kuongeza thamani.

Akiwa katika mradi wa Kilimo cha Vitunguu katika Kata ya Mang’ola, Mongella amewaaidi kuwasaidia wakulima hao, masoko ya uhakika ili kilimo hicho kiwe cha tija na manufaa kwao na Taifa zima kwa ujumla.

Amesema, Serikali imewekeza fedha nyingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo ili wananchi waweze kupata huduma bora na kwa ukaribi zaidi.

Hata hivyo, amewataka wananchi kuithamini na kuitunza miradi hiyo kwani ipo kwa ajili yao na itawapatia huduma muhimu na kwa ukaribu zaidi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Dadi Holace Kolimba amesema Wilaya inashirikiania kwa ukaribu na viongozi wa Halmashauri, ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa haraka kama ilivyokusudiwa.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Karia Rajabu amesema watayasimamia maelekezo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa, ili Halmashauri hiyo iweze kukamilisha miradi yote ya maendeleo kwa wakati.

Katika ziara hiyo, Mongella amekagua ujenzi wa majengo katika shule ya Sekondari Ayalabe yaliyogharimu Milioni 470 kwa awamu ya kwanza na ujenzi wa majengo katika Hospitali ya Wilaya ya Karatu yenye thamani ya Shilingi 2.4 Bilioni

Miradi mingine ni upandaji na uvunaji wa Vitunguu katika Shamba la Mang’ora na ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje, maabara, jengo la wazazi na upasuaji lililogharimu shilingi Milioni 250 katika kituo cha Afya Mbuga nyekundu.

UN yaalaani mauaji watu 22 Ukraine
Wazazi CCM watakiwa kujenga heshima za Viongozi