Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ghana Bernard Morrison ameanza kuitia hofu Jwaneng Galaxy, kuelekea mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa ligi ya Mabingwa Barani Afrika, hatua ya Kwanza utakaochezwa mwishoni mwa juma hili mjini Gaborone, Botswana.

Simba SC itaanzia ugenini Oktoba 17, kisha itarejea nyumbani jijini Dar es salaam tayari kwa mchezo wa Mkondo wa pili uliopangwa kucheza Oktoba 22, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Jina la Morrison limetajwa na Kocha Mkuu wa Jwaneng Galaxy Morena Ramoreboli, kama mmoja wa wachezaji hatari wa Simba SC na anatakiwa kuchungwa sana kwenye michezo yote miwili.

Kocha Morena amesema kikosi cha Simba kimesheheni wachezaji wazuri huku akimtaja Kiungo Mshambuliji Bernard Morrison kuwa ndiye mchezaji tishio ambaye aliwahi kumshudia wakati akiwa anakipiga katika klabu ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini jambo ambalo anaamini wachezaji wake wanatakiwa kuwa makini wakati wote.

“Licha ya ubora wa Simba kama timu lakini ina wachezaji wengi wazuri mmoja namfahamu vyema ni Bernard Morrison kwa kuwa nilimshuhudia akiwa katika klabu ya Orlando Pirates ya nchini Afrika Kusini.”

“Ni mchezaji mzuri na mwenye kasi ambaye anahitaji ulinzi mzuri ili asilete madhara, kwa upande wetu tunafahamu kuwa tunaenda kucheza na timu bora hivyo tutahitaji kuonyesha ubora wetu dhidi yao ili tushinde mchezo tukiwa nyumbani,”amesema Kocha Morena Ramoreboli.

Mshindi wa Jumla wa mchezo huo atatinga hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, huku atakayepoteza atashuka kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho na kucheza michezo ya mtoano kabla ya kutinga hatua ya Makundi.

Tyga aingia matatani baada ya kumtembezea kichapo mpenzi wake.
Simba SC kuwashtukiza Jwaneng Galaxy