Mwenyekiti wa Bodi ya Parole ya Taifa, Dkt. Augustine Lyatonga Mrema amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufanikisha safari ya kwenda nchini India kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa afya yake.

Mrema ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uteuzi uliofanywa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Lameck Nchemba kwa kuwateua wajumbe wawili wa bodi hiyo.

“Nachukua nafasi hii kumshukuru Rais Magufuli , Waziri Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Wizara ya Afya na Ikulu, kwa kunipeleka nchini India kufanyiwa uchunguzi wa afya yangu na kupatiwa matibabu na sasa afya yangu imeimarika na niko tayari kutekeleza majukumu yangu,” amesema Mrema.

Aidha, akizungumzia uteuzi uliofanywa na Waziri Nchemba, Mrema amesema kuwa toka alivyoteuliwa na Rais Magufuli kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Parole Taifa, Bodi hiyo haikukaa vikao kutokana na baadhi ya wajumbe wa Bodi hiyo kumaliza muda wao.

Mrema amewataja walioteuliwa kuwa wajumbe wa Bodi ya Parole Taifa ni pamoja na Francis Kistola na John William Nyoka.

Hata hivyo, Mrema amempongeza Waziri wa Mambo ya Ndani kwa kukamilisha kazi ya uteuzi na amewapongeza wajumbe walioteuliwa na kuwakaribisha kwa mikono miwili kwenye bodi hiyo na kuomba ushirikiano wao na uzoefu wao ili kukamilisha majukumu ya bodi ya Parole.

 

Wasanii tumieni kiswahili katika kazi zenu-Prof. Elisante
Ujenzi wa Ubungo Interchange kuanza mara moja