Mwenyekiti wa Tanzania Labor Party (TLP), Augustine Mrema ameishauri Serikali kumtia nguvuni, Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad na kumfungulia mashtaka ya uhaini.

Mrema alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu  msimamo wa chama chake juu ya usalama na hali ya kisiasa visiwani Zanzibar baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa marudio.

Alisema kuwa kauli ya Maalim Seif kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein hatamaliza kipindi chake cha uongozi na kwamba yeye ndiye atakayekuwa Rais ni kinyume cha sheria na inaashiria uhaini.

Alivitaka vyombo vya usalama kumchukulia hatua sitahiki kwani kauli zake ni hatari kwa usalama wa nchi.

“Wote tunafahamu kuwa uchaguzi wa Oktoba ulifutwa kwa mujibu wa sheria na ulifutwa na nani (Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar), na kwamba uchaguzi wa marudio ulifanyika na Rais Ali Mohammed Shein ndiye aliyeshinda,” alisema Mrema.

Alisema kuwa chama chake kimeamua kuzungumza kwakuwa ni chama cha siasa na kinapaswa kukemea hali yoyote inayohatarisha amani ya nchi.

Mrema alisisitiza kuwa amani ya Zanzibar ni muhimu kwani endapo itaharibika hata Tanzania Bara haitakuwa salama.

Cannavaro Asafiri Na Taifa Starts Hadi Nairobi - Kenya
Video: Trilion 1.3 zilizoombwa na Wizara ya Elimu na Mgawanyo Wake

Comments

comments