Rais wa Jamhuri ya Uganda, Yoweri Museveni ametoa wito wafanyabiashara wa Kitanzania kwenda kuwekeza nchini Uganda, Museveni ametoa kauli hiyo leo wakati alipotembelea viwanda vya Kampuni ya  Bakhresa vinavyozalisha Unga na Juisi  vya  Buguruni na Vingunguti jijini Dar es Salaam.

“Nawakaribisha  wafanyabiashara wa Kitanzania kuja nchini Uganda kuwekeza kwani kufanya hivyo kutasaidia kuzalisha bidhaa, upatikanaji wa soko pamoja na ajira” amesema Museveni.

Aidha, kauli hiyo ya Rais Museveni imetokana na mafanikio yanayotokana na Mwekezaji wa Kitanzania Said Salim Bakhresa aliyewekeza nchini Uganda ambapo anamiliki Kiwanda cha kusanga ngano nchini humo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa  Mahusiano wa Kampuni za Bakhresa, Hussin Sufiani amesema kwamba Kampuni hiyo iko mbioni kuongeza uzalishaji wa unga wa ngano kutoka tani 1,100 hadi kufikia tani 2,000 kwa siku nchini Uganda.

Aidha, amesema kutokana na uwekezaji wa Kampuni hiyo nchini Uganda jumla ya Waganda 650 wamenufaika na ajira mbalimbali ambazo zinasaidia kuwapatia kipato.

Kwa upande wa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji. Charles Mwaijage amesema kuwa Uganda na Tanzania zimeingia makubakliano  ya ushirikiano katika sekta mbalimbali  ikiwemo sekta ya viwanda.

“Tunawahamasisha wafanyabiashara wa Uganda na Tanzania kuwekeza katika nchi zao ili kuzalisha , bidhaa na ajira za kutosha kwa wananchi” amesema Waziri Mwijage.

Pia Mwijage ametoa Wito kwa Watanzania kushiriki katika uchumi wa viwanda kwa kufanya uzalishaji wa bidhaa zinazotumika viwandani mfano kwa kulima matunda au mbogamboga.

Rais Yoweri Museveni aliwasili nchini jana kwa ziara ya kiserikali ya siku mbili ambapo akiwa nchini amefanya mazungumzo na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na kutembelea Viwanda vya  Said Salim Bakhresa vya Tazara na Vingunguti.

Kamanda Sirro aelezea changamoto anazokutana nazo
DC Hapi aagiza Jeshi la Polisi kumuweka ndani Afisa uthamini wa Kinondoni