Mechi ya kwanza kabisa ya Sudan Kusini katika kampeni ya kufuzu kwa Kombe la Dunia ilisitishwa kutokana na mvua kubwa baada ya kuchezwa dakika 10 pekee.

Mechi hiyo ya mkondo wa kwanza iliyokuwa ikichezewa mjini Juba ilisimamishwa mambo yakiwa 1-1 kati yao na Mauritania.

Licha ya kuchezwa muda huo mfupi, Sudan Kusini bado walifanikiwa kupata la kujivunia kwa kufunga bao lao la kwanza kabisa kinyang’anyiro cha Kombe la Dunia.

Bao lao walifungiwa na Dominic Abui Pretino dakika ya tano na kukomboa bao lililokuwa limefungwa na Boubacar Bagili dakika ya tatu.

Fifa imesema mechi hiyo itarejelewa saa tano leo.

Mataifa hayo mawili yanatarajiwa kukutana tena kwa mechi ya marudiano mjini Nouakchott Jumanne Oktoba 13.

South Sudan ilianza kucheza soka ya kimataifa 2012, mwaka mmoja baada ya kupata uhuru kutoka kwa Sudan.

Mwezi uliopita, waliandikisha ushindi wao wa kwanza kabisa mechi ya ushindani walipolaza Equatorial Guinea 1-0 mechi ya kufuzu kwa Kombe la Taifa Bingwa Afrika 2017.

Haya hapa ndiyo matokeo ya mechi nyingine za kufuzu kwa Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi zilizochezwa Jumatano:

Ushelisheli 0-1 Burundi

Tanzania 2-0 Malawi

Comoros 0-0 Lesotho

Mauritius 2-5 Kenya

Mzee Kingunge Kupanda Jukwaa La Ukawa Jijini Arusha, Leo
Sepp Blatter Afungiwa Kwa Siku 90