Licha ya kupigwa kwa Technical Knock Out (TKO), Hassan Mwakinyo amepanda kwa nafasi mbili katika viwango vya ubora wa ngumi za kulipwa vya dunia.

Kwa mujibu wa mtandao wa ngumi wa dunia (Boxrec), Mwakinyo sasa ni bondia wa 38 kati ya 1,953 duniani kwenye uzani wa super welter akipanda kwa nafasi mbili kutoka ya 40 aliyokuwa awali kabla ya pambano na Liam Smith.

Mwakinyo alizichapa na Smith Septemba 3 nchini Uingereza na kupigwa kwa TKO ya raundi ya nne, kabla ya Boxrec kumtaja kupanda kwenye ubora kwa nafasi mbili, akibebwa na nyota tatu na nusu na pointi anazomiliki kwa sasa katika ubora huo.

Katika viwango hivyo, Wamarekani, Jermell Charlo na Sebastian Fundora ndio vinara wakikamata namba moja na mbili ya dunia wote wakiwa na nyota tano na Magomed Kurbanov akihitimisha tatu bora ya dunia.

Smith ameendelea kusalia kwenye nafasi yake ya awali ya sita huku Sam Eggington aliyewahi kuchapwa na Mwakinyo kwa TKO mwaka 2018 akiangukia kwenye nafasi ya 13.

Katika viwango vya Afrika, Mwakinyo ameendelea kusalia kwenye nafasi ya pili nyuma ya kinara Roarke Knapp wa Afrika Kusini ambaye amekuwa kwenye nafasi hiyo kwa zaidi ya miezi sita sasa tangu Mwakinyo alipoporomoka.

Awali Mwakinyo ndiye alikuwa kinara kuanzia 2018 alipomchapa Eggington, ingawa miezi sita iliyopita aliporomoka hadi nafasi ya pili ambako ameendelea kusalia hadi sasa kwenye uzani wake.

Brandon Thysse pia wa Afrika Kusini amehitimisha tatu bora kwa uzani huo barani Afrika akimshusha Mcongo, Emmany Kalambo ambaye katika viwango vipya ameporoka hadi nafasi ya nne.

Nyota wengine Watanzania, Mfaume Mfaume na Meshack Mwankemwa wameingia kwenye 20 bora katika uzani huo, Mfaume akiwa wa 15 na Mwankemwa wa 16 huku Nicolaus Michael Mdoe akitajwa kwenye nafasi ya 20.

Chanzo: Mwanaspoti

Watatu Young Africans kuikosa Zalan FC
Simba SC yafunguka hatma ya Dejan Georgijevic