Katika hali isiyo ya kawaida, mwanaume mmoja aliyejitambulisha kama mwimbaji wa nyimbo za injili alyekamatwa kwa kosa la ujambazi wa kutumia silaha, amedai kuwa alishiriki uhalifu huo kupata fedha za kulipia albam yake studio.

Jeshi la Polisi nchini Nigeria limemtaja kijana huyo kwa jina la Nurudeen Ogundairo mwenye umri wa miaka 28, aliyekamatwa akiwa na vijana wawili ambao walijitambulisha kama wapiga vyombo wa bendi yake ya muziki wa injili. Vijana hao pia walikamatwa kwenye tukio la ujambazi pamoja na bosi wao.

Ogundairo alidai kuwa alipanga kufanya uzinduzi wa albamu yake Julai 24 mwaka huu lakini hakuwa na fedha kwa ajili ya kulipia utengenezaji wake na uzinduzi.

“Kwakweli nilipanga Julai 24 kuwa siku ambayo ningezindua albam yangu kwa umma baada ya kulipia utayarishaji wake. Nilijiingiza kwenye ujambazi ili nipate fedha za kuwezesha mradi wangu wa albam,” alisema.

Mtuhumiwa huyo alieleza kuwa baada ya kukaa selo kwa miezi miwili amejifunza mengi na anaomba asamehewe.

“Ninaamini Jeshi la Polisi pamoja na Mungu watanisamehe kwa makosa yangu niliyoyafanya. Nilidanganyika na tamaa za kutaka kufanikiwa kwenye muziki wangu wa injili ndio maana nilijihusisha na ujambazi,” anakaririwa.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya kuaminika vya Nigeria, vijana wengine waliokamatwa pamoja naye kwa tuhuma za ujambazi walitajwa na Jeshi la Polisi kuwa ni Tunde Joseph na Ganiu Ajibode.

Serikali yapunguza gharama za umilikaji ardhi
Video: Madareva 24 waliotekwa DRC, Wizara ya Mambo ya Nje yatoa tamko