Kocha wa Polisi Tanzania, Mwinyi Zahera amewatoa hofu mabosi wa timu hiyo kwa kuwahakikishia atainusuru isishuke daraja na msimu ujao itacheza Ligi Kuu Tanzania Bara.

Polisi Tanzania tayari imeshawasili mjini Dodoma kwa ajili ya mchezo wa Ligi Tanzania Bara utakaopigwa Uwanja wa Jamhuri dhidi ya Dodoma Jiji kesho Jumapili (Machi 12).

Zahera alitangazwa Kocha Mkuu akichukua nafasi ya Joslin Sharif, aliyetimuliwa Oktoba 17 sambamba na msaidizi wake, Augustino Damian na timu kuwa chini ya John Tamba kwa muda ambaye awali alikuwa kocha wa viungo.

Tangu Desemba 02-2022, alipotangazwa kuwa Kocha Mkuu timu hiyo imecheza michezo 10 akishinda michezo miwili, ilipoichapa mabao 2-0 Namungo FC kisha ikaifunga Tanzania Prisons bao 1-0, sare nne na kuchapwa michezo minne.

Afisa Habari wa timu hiyo, Frank Lukwaro amesema Zahera amewahakikishia kupambana ili kukwepa kushuka daraja kwani wanashika nafasi ya 15 wakiwa na alama 19.

“Kitu kikubwa ambacho kocha alisema kuna tatizo eneo la ushambuliaji ambapo nafasi nyingi zilizokuwa zikipatikana zilikua hazizai matunda mazuri.”

“Baada ya majuma mawili kukaa bila mchezo ameyafanyia kazi mapungufu hayo na kuahidi matokeo mazuri katika michezo inayofuata tukianza na Dodoma Jiji wiki hii,” amesema Lukwaro.

Ameongeza bado hawajakata tamaa na matumaini ya kubaki Ligi Kuu, kwani wana kila sababu ya kuitumia michezo iliyosalia kupata alama zitakazowanusuru na nafasi za juu katika msimamo.

Lukwaro amesema uongozi wa timu unapambana kuona wanakamilisha stahiki zote za wachezaji na Benchi la Ufundi ili wachezaji wanatimiza vyema majukumu yao uwanjani.

Baada ya mchezo huo Polisi itakuwa imesalia na michezo mitano dhidi ya Singida Big Stars, Ihefu FC, Mtibwa Sugar, Simba SC kisha itamaliza msimu kwa kucheza na Azam FC.

Polisi Tanzania ilipanda Ligi Kuu msimu wa mwaka 2019/20 pamoja na Namungo FC ikiwa chini ya Mbwana Makata ambaye baada ya hapo alikwenda kuipandisha Dodoma Jiji FC (2020/21).

Kifo cha Mobby chapeleka ujumbe TFF
Shomari Kapombe afichua siri nzito