Sintofahamu iliibuka jana Bungeni baada ya Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson kumkanya Mbunge kwa kumuita Bwege huku akimtaka kutoleta ‘ubwege’ katika nyumba hiyo ya Wawakilishi wa Wananchi.

Dk. Tulia alitumia neno ‘bwege’ kwa Mbunge wa Kilwa Kusini, Selemani Saidi Bungara (CUF), baada ya mbunge huyo kusimama bila kufuata kanuni za Bunge na kuanza kupinga maelezo ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye aliyekuwa akijibu hoja za Bunge kutorushwa moja kwa moja kupitia vituo vya Runinga.

“Na wewe Mheshimiwa Bwege, hebu kaa chini. Usionyeshe ubwege wako hapa,” alisema Dk. Tulia katika jitihada za kurudisha Bunge kwenye utulivu wake.

Mbunge mmoja wa Ukawa aliwasha kikuza sauti chake na kusema, “Hatimaye msamiati wa bwege watua bungeni sasa kutumika rasmi. Futa lugha ya kuudhi; bwege bwege.”

Wabunge hao walikumbushia kesi ya kijana aliyekamatwa jijini Arusha hivi karibuni na kufikishwa mahakamani kwa kosa la kuandika kwenye mtandao lugha ya kuudhi dhidi ya Rais Magufuli akimuita ‘bwege’.

Naye Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa alisimama kupinga taarifa iliyotolewa na Nape huku akimtahadharisha Naibu Spika kwa kauli yake ya kumuita mbunge bwege na kwamba angepeleka mahakamani.

“Taarifa yake naikataa kwa sababu anasema uongo. Leo na wewe umemuita mtu bwege. Kuna mtu kule Arusha alimuita Rais Magufuli bwege na akapelekwa mahakamani. Na wewe tutakupeleka mahakamani,” alisema Msingwa.

Hata hivyo, Mbunge huyo wa CUF katika Bunge la Kumi alijitambulisha bungeni humo kuwa yeye hufahamika kwa jina maarufu la ‘Bwege’.

 

 

George Weah Atangaza Tena Kuwania Urais
Chadema wasusia Mchakato wa Katiba Mpya inayopigiwa chapuo