Waziri Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Ummy Mwalimu amewaagiza Makatibu Tawala wa Mkoa kote nchini kuhakikisha wanafanya msawazo kwa watumishi wote wakiwemo wa sekta ya afya ili kupunguza uhaba wa watumishi katika maeneo yao.

Ameyasema hayo leo wakati alipokuwa akikagua ujenzi wa Hospiatali ya Wilaya ya Kibiti katika ziara ya kikazi aliyoifanya katika, Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani kwa ajili ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri hiyo.

Katika hatua nyingine Waziri Ummy amesema jumla ya shilingi bilioni 53.6 zitatolewa na Serikali kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Hospitali za Wilaya 67 zilizojengwa nchini.

Waziri Ummy amesema kuwa katika kuhakikisha Hospitali za Wilaya zilizojengwa katika awamu ya kwanza zinakamilika serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 800 kwa kila Hospitali ya Wilaya lengo likiwa ni kukamilisha miundombinu ya majengo katika hospitali hizo

Aidha katika awamu ya kwanza ya ujenzi serikali ilipeleka fedha kiasi cha shilingi bilioni 1. 5 kwa ajili ya ujenzi wa majengo saba ya awali, kisha shilingi milioni 300 na sasa shilingi milioni 800 kwa ajili ya ukamilishaji wa miundombinu hiyo ili wananchi waweze kupata huduma bora za afya katika maeneo yao.

Aidha, amesema kuwa Serikali imejipanga katika kuhakikisha vifaa na vifaa tiba vinapatikana kwa wakati ili wananchi waweze kuzitumia Hospitali zetu kikamilifu kwa kuhakikishiwa kuwa huduma bora zinapatikana katika Hospitali za Serikali.

Madaktari wapendekeza chanjo ya Uviko 19 kuwa lazima
Azam FC wamaliza maandalizi