Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga ameihusisha familia ya Rais Uhuru Kenyatta na ufisadi wa shilingi bilioni 5.3 za Kenya za Wizara ya Afya ya nchi hiyo.

Akihutubia katika mkutano na waandishi wa habari jana jijini Nairobi, Odinga ambaye ni kiongozi wa CORD alidai kuwa katika ufisadi huo, dada yake Rais Kenyatta aitwae Nyokabi Muthama na binamu yake Kathleen Kihanya ambaye alikuwa kwenye timu yake ya Kampeni, wamehusika moja kwa moja na ufisadi huo.

Taarifa za ufisadi huo zimeanza kusambaa kutokana na kuvuja kwa ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali katika Wizara ya Afya, ripoti iliyothibitishwa kuwa ya kweli.

“Sakata hili la ufisadi ni la Rais Kenyatta. Anapaswa kulifanyia kazi kwa namna hiyo. Ni lazima aieleze nchi anachokifahamu, lini alikifahamu na alifanya nini baada ya kufahamu hilo,” alisema Odinga.

Alisema kuwa kwa mujibu wa ripoti hiyo, makampuni yaliyohusika katika kufanya manunuzi ya wizara hiyo ambayo ni ya kifisadi, yanaonekana kuwa na ushirika wa karibu na familia hiyo ya Rais na wengine wakiwa na marafiki zake.

“Rais hawezi kudai kuwa hafahamu chochote kuhusu watu hawa. Na Kenya inajua watu hawa ni akina nani kwa Rais,” alisema.

Ikijibu tuhuma hizo, Wizara ya Afya kupitia Katibu Mkuu wake, Cleopa Mailu ilieleza kuwa ilikuwa inaifanyia kazi kwa uzito unaostahili ripoti hiyo ambayo ilivuja kwa vyombo vya habari kabla haijawekwa wazi rasmi.

“Tuhuma hizo zimejikita katika ripoti ya ukaguzi ambayo tunakiri na kutambua kuwa iko katika mchakato unaoendelea, ambayo ilivuja kwa vyombo vya habari kabla wakaguliwa hawajajibu tuhuma zilizotajwa dhidi yao kwenye ripoti husika,” imeeleza taarifa ya Wizara hiyo.

Wizara hiyo imesisitiza kuwa ripoti hiyo itafanyiwa kazi kwa uwazi usawa unaostahili.

Makonda awaasa wazazi kutowachagulia masomo wanafunzi
Shinyanga walilia mkaa rafiki kwa mazingira