Dar es salaam, Zikiwa zimebakia siku nane kabla ya kuzinduliwa kwa operesheni ya umoja wa kupinga Udikteta Tanzania (UKUTA),  jeshi la Polisi limelegeza masharti ya kudhibiti shughuli za kisiasa baada ya kuruhusu mikutano ya ndani ya vyama na ya wabunge kwenye majimbo yao.Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Nsato Mssanzya ametangaza kuondoa zuio hilo.

Lakini Chadema, ambayo ilianzisha operesheni hiyo, imesema pamoja na jeshi la polisi kulegeza masharti, iwapo viongozi wa dini na Rais Magufuli hawatafikia muafaka kuhusu madai yao, msimamo wao wa kuendesha mikutano na maandamano kuanzia Oktoba Mosi uko palepale. Naibu Katibu Mkuu wa Chadema – Zanzibar, Salum Mwalimu aliongea na vyombo vya habari .

”Kama tulivyosema tangu awali Ukuta ni suala endelevu. Siku zimebakia chache, lakini tunasubiri kusikia viongozi wa dini wanasemaje ili kujua tunaanza kuhesabu kufikia Ukuta au kuufuta kabisa ,” alisema Mwalimu.

Chadema ilitangaza operesheni hiyo  Julai 27 kupinga kile inachokiita, ”Serikali kutoheshimu katiba na sheria na kukandamiza demokrasia,” ikiwa ni pamoja na kuzuia mikutano ya kisiasa.

Miongoni mwa viongozi wa dini wanohusika katika mazungumzo hayo Mufti wa Tanzania , Sheikh Mkuu Abubakar Zubeir ambaye alisema maridhiano yanahitaji subira , ikizingatiwa kwamba yanahusisha serikali na kwamba wakati mwingine mambo tofauti hujitokeza katikati.

Mwenyekiti wa kamati ya uongozi CUF, Julius Mtatiro alimtaka Rais Magufuli atamke hadharani kwamba alifanya makosa kuzuia mikutano hadharani kwani haki ya vyama vya siasa kufanya mikutano hadharani  ni ya kikatiba na haiwezi kuondolewa.

Waziri Mkuu apokea sh. Mil. 172.5 kwa ajili ya waathirika tetemeko Kagera
Video: Aliyegundua muonekano mpya wa Bodaboda aipongeza Serikali