Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli  ameendelea na ziara yake Visiwani Zanzibar ambapo majira ya Asubuhi amezuru Kaburi la Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Marehemu Sheikh Abeid Amaan Karume lililopo kando ya Ofisi Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) eneo la Kisiwandui Zanzibar.

Rais Magufuli akiwa na Mkewe Mama Janeth Magufuli wameweka mashada ya maua katika Kaburi hilo na baadaye wameshiriki Dua ya kumuombea Marehemu Sheikh Abeid Amaan Karume na kuombea amani.

Viongozi mbalimbali wa Dini na Siasa akiwemo Rais Mstaafu wa Sita wa Zanzibar Dkt. Amani Abeid Karume na familia ya Hayati Sheikh Abeid Amaan Karume ikiongozwa na Mjane wa Marehemu Mama Fatma Karume wamehudhuria.

Baada ya kuzuru kaburi la Marehemu Sheikh Abeid Amaan Karume, Rais Magufuli amezuru kaburi la Rais wa Pili wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Marehemu Aboud Jumbe Mwinyi lililopo nyumbani kwake Migombani Zanzibar.

Dkt. Magufuli na Mkewe Mama Janeth Magufuli wameweka mashada ya maua katika kaburi la Marehemu Aboud Jumbe Mwinyi na pia wametoa mkono wa pole kwa familia ya Marehemu.

Wakizungumza katika Dua ya kuwaombea Marehemu wote wawili Viongozi wa Dini kutoka madhehebu ya Kiislamu na Kikristo wameomba kuwepo kwa amani na upendo kwa watanzania wote kama ambavyo waasisi wa Taifa walipigania.

RPC awatoa wananchi hofu ya Ugaidi, ni baada ya Hostel kuvamiwa Tanga