Serikali imetoa nafasiya kurudi shule kwa wanafunzi walioacha shule kwa sababu mbalimbali za kibinadamu ikiwemo sababu za kiuchumi, kupata ujauzito na wale walioacha na kujutia baadae ili kutoa fursa ya elimu kwa wote nchini Tanzania.

Hayo yameyasemwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika hafla ya makabidhiano ya Shule ya Awali na Msingi ya Museven wilayani Chato ambayo yamefanyika baina ya Rais wa Uganda Yoweri Museven na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

“Nataka kutoa ufafanuzi kwa wale wanaojadili swala la watoto wa kike waliopata ujauzito kurudi shule, sisi hatutasema hao tu ila wote walioacha kwa sababu zote za kibinadamu na baadae wakajutia. Hapo kuna wale ambao tumewaanzishia shule mbadala watakazojifunza namna ya kuendesha maisha yao ya baadae, hivyo niweke sawa msijadili kwa kuangalia upande mmoja ila kwa kuona umuhimu wa elimu kwa wote” Amesema Rais Samia.

Rais Samia pia amemuomba Rais Museven kuweka shule ya muendelezo wa elimu huko nchini Uganda ambayo itasaidia wanafunzi wanaomaliza darasa la 7 katika shule hiyo ya Museven wapate nafasi ya kujiendeleza kwa lugha ya kiingereza nchini Uganda.

Katika Makabidhiano hayo Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museven ametoa ufafanuzi kuwa hakujenga shule hiyo kwa sababu Tanzania haina uwezo ila ni kwa sababu ya kuacha kumbukumbu na kusaidia kukuza elimu ya Nchi Tanzania.

“Nimekua nikifanya vitu vya maendeleo kila ninapofika nchini Tanzania kuanzia uongozi wa Rais Mkapa, hivyo shule hii nimeijenga kw akumuomba Marehemu Magufuli na alikubali niijenge kwa kuendeleza mahusiano mazuri, na sio yeye alieniomba” alifafanua Rais Museven.

Pia amemuomba Rais Samia awaelekeze JWTZ kusimamia shule zilizojengwa nae wakati wa nyuma kwa sababu walishirikiana vizuri katika mapigano wakati wa kupigania uhuru wa Uganda na Tanzania.

Nae Waziri wa Elimu Profesa Joyce Ndalichako amesema serikali imeongeza nafasi kwa wanafunzi wanaofeli mitihani ya darasa la 7 kwa mara ya kwanza kurudia mtihani kwa mara nyingine na endapo watafaulu watapangiwa shule za sekondari za serikali ili kuendeleza mpango wa elimu kwa wote.

Awali Naibu waziri wa Ofisi ya Rais TAMISEMI David Silinde akizungumza katika uzinduzi huo amesema katika harakati za kudumisha elimu msingi kabla ya tarehe 15 ya mwezi Disemba madarasa elfu 15 yatakua yamekamilika kwa fedha za UVIKO 19 zilizotolewa na Rais Samia.

Mkoa wa Geita una shule za msingi 701, ikiwa shule 652 ni za serikali na zinazofundisha lugha ya kingereza ni shule 52 ikiwemo shule mpya ya Museven inayomilikiwa na Serikali.

Shule ya Awali na Msingi ya Museven wilayani Chato, Geita ilianza kujengwa mwezi Februari 2020 na imekamilika February 2021, ikiwa na madarasa 20, Jengo moja la utawala, Matundu 37 ya vyoo, ofisi 2 na nyumba za walimu na inatarajia kuanza kupokea wanafunzi mwezi januari 2022.

Nabi ahofia uwanja wa Sokoine
Uzinduzi shule ya Msingi Museveni-Chato