Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF)-Bara, Magdalena Sakaya ambaye Baraza Kuu la Chama hicho lilitangaza miezi mitatu iliyopita kumvua uanachama, ametaja kiini na tiba ya mgogoro mkubwa unaokitafuna chama hicho hivi sasa.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Dar24, Sakaya ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Kaliua, amesema kuwa mgogoro huo kwa asilimia 90 umetokana na mvutano wa ndani wa muda mrefu kati ya Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili, Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.

Amesema kuwa mpasuko huo haukutokana na suala la CUF kumuunga mkono aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema kupitia Ukawa, Edward Lowassa kama wengi wanavyoamini, na kwamba suala hilo lilichangia tu kulipua tofauti za ndani za muda mrefu kati ya viongozi hao.

Alisema uamuzi wa kumfukuza uanachama Profesa Lipumba ni uamuzi binafsi wa Maalim Seif akilitumia Baraza Kuu.

“Tunasema yale ni maamuzi ya mtu mmoja kwa sababu gani, tunamjua Maalim, tumefanya naye kazi… ni kiongozi ambaye anapenda neno lake liwe la mwisho,” Sakaya aliiambia Dar24.

“Wenye uwezo wa kuumaliza huu mvutano ni watu wawili tu, Lipumba na Maalim. Maalim ana nguvu Zanzibar, na Lipumba ana nguvu Bara. Kila mmoja akikaa na watu wake, tukaja kwenye meza moja, wakakubaliana pamoja kwamba tumeshakubaliana kukaa na kudumisha chama chetu, wafuasi wao wote watasikiliza,” alisema.

Katika hatua nyingine, Sakaya alieleza kutokubaliana na uamuzi wa kuvuliwa uanachama na Baraza hilo kwakuwa mkutano huo haukufuata katiba ya chama hicho na kwamba waliouitisha walikuwa na ajenda ya siri.

Baraza Kuu la CUF linamshtaki Mahakamani Profesa Ibrahim Lipumba na Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, Jaji Francis Mutungi aliyeandika barua ya kumtambua mwanasiasa huyo kama Mwenyekiti halali wa chama hicho.

Baraza hilo linaiomba Mahakama kumzuia Msajili kuingilia maamuzi ya chama pamoja na kubatilisha barua yake.

Video: Lyaniva azitaka taasisi za kidini kujitolea damu
Makonda atoa agizo kwa watendaji wa kata