Kiungo na Nahodha wa Timu ya Taifa ya Hispania ‘La Roja’ Sergio Busquets ameshikwa na kigugumizi kuhusu mustakabali wa kuendelea ama kustaafu kuitumikia timu hiyo, baada ya Fainali za Kombe la Dunia 2022, zinazoendelea nchini QATAR.

Kiungo huyo wa FC Barcelona anashiriki kwa mara ya nne mfululizo katika Fainali za Kombe la Dunia, kwa mara ya kwanza alikuwa kwenye kikosi kilichotwaa ubingwa wa Fainali hizo Afrika Kusini mwaka 2010.

Busquets mwenye umri wa miaka 34 pia alikuwa kwenye kikosi cha Hispania kilichotwaa Ubingwa wa Fainali za Ulaya ‘Euro 2012’, huku akiweka malengo ya kulisaidia taifa lake kutwaa Ubingwa wa Dunia mwaka huu 2022.

“Nina furaha sana kuwa hapa, bila kujali ikiwa ni Fainali za ngapi kwangu, Sitafanya maamuzi kustaafu kuitumikia Hispania baada ya Fainali hizi ama baadae, ninatakiwa kueleweka kuwa nitaendelea kuwa sehemu ya timu hii,”

“Niko hapa kufurahia chochote kitakachotokea. Ni wazi kuwa niko karibu na hili kuwa Kombe langu la mwisho la Dunia.” amesema Busquets

Timu ya Taifa ya Hispania itaanza Kampeni ya kusaka Ubingwa wa Dunia kwa kuivaa Costa Rica katika mchezo wa Kundi E, utakaopigwa Uwanja wa Al Thumama mjini Doha, kesho Jumatano (Novemba 23).

Hispania wamekua na mwanzo mbaya katika Michuano mikubwa kwa miaka ya karibuni ambayo yote Busquets alicheza, na alipoulizwa kuhusu hilo alisema: “Ni wakati sasa wa kuanza kwa kupata ushindi.”

“Ni wazi tunajua itakuwa ngumu, lakini lengo letu ni kucheza michezo saba bila kupoteza, kupambana hadi mwisho na kwa nini tushindwe? Tunahitaji kwenda hatua kwa hatua.”

“Katika michuano yangu yote ya Kombe la Dunia hatujashinda mchezo wa kwanza. Tukishinda itakuwa vizuri sana kwetu kufanya Kundi liwe shwari zaidi baada ya hapo.”

“Ukishinda mchezo huu wa kwanza ni rahisi kuendelea.” amesema

HABARI ZA TIMU
Beki wa kushoto wa Hispania Jose Gaya aliondolewa kwenye kikosi cha michuano hiyo, baada ya kuumia kifundo cha mguu akiwa mazoezini.

Nafasi yake imechukuliwa na chipukizi wa FC Barcelona Alejandro Bald, lakini hakuna majeruhi wengine kwenye kikosi cha Hispania.

Kwa upande wa Costa Rica wachezaji wote wanaounda kikosi cha nchi hiyo wapo FIT kuikabili Hispania kesho Jumatano (Novemba 23).

Boti yapotea, waokoaji wahaha kuitafuta
Serikali kutathmini upya utendaji wa TCRA-CCC