Serikali kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), imetolea ufafanuzi taarifa zilizosambaa na zilizoandikwa na gazeti la Jambo Leo la Juni 24 mwaka huu kuwa ‘Serikali imeamua kupima Ukimwi Nyumba kwa Nyumba’.

NBS imekanusha taarifa hizo na kueleza kuwa mpango wa Serikali sio kupima Ukimwi nyumba kwa nyumba, bali ni kufanya utafiti kuhusu viashiria na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi nchini kuanzia mwezi Septemba mwaka huu.

Taarifa ya NBS kwa vyombo vya habari imeeleza kuwa katika utafiti huo, wamechagua kisayansi kaya 16,000 ambazo zitatumika kama sampuli katika Tanzania Bara na Zanzibar ili kupata matokeo yenye uwakilishi wa kaya zote ambazo hazitashiriki moja kwa moja.

NBS imesema kuwa sampuli hiyo imelenga pia kuwapima watu wazima wasiopungua 40,000 na watoto 8,000.

Mbali na Ukimwi, utafiti huo pia utalenga katika kutafuta taarifa za magonjwa mbalimbali na mfumo wa damu.

“Katika utafiti huu pia kutakuwa na kupima homa ya ini, kupima wingi wa chembechembe za damu yaani CD4, kupima wingi wa virusi katika damu na kupima kiwango cha ufanisi wa dawa za kufubaza VVU kwa watu wanaotumia dawa hizo,” imeeleza taarifa hiyo.

Hii sio mara ya kwanza kufanyika kwa utafiti wa aina hiyo, kwani Serikali ilifanya utafiti huo kwa kutumia mtindo huo wa sampuli mwaka 2003, 2007 na 2011.

Mabomu ya Kigaidi yaua makumi uwanja wa ndege Uturuki
Akamatwa kwa kuweka nyeti zake kwenye 'scanner' ya ukaguzi 'Supamaketi'