Na Baraka Mbolembole

Kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka mitatu timu ya Simba SC itakuwa na nafasi ya kuongoza msimamo wa ligi kuu Tanzania bara, hilo litawezekana endapo mabingwa hao wa zamani watapata ushindi katika mchezo wa wikendi hii dhidi ya Stand United katika uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Mara ya mwisho kwa ‘Wekundu wa Msimbazi’ kuongoza msimamo wa ligi kuu ni mwanzoni mwa msimu wa 2013/14 wakiwa chini ya kocha Abdallah ‘King’ Kibadeni na Jamhuri Kiwhelo’ ‘Julio’ ambao waliiongoza timu hiyo kushinda michezo mitano mfululizo ya mwanzo mwa msimu.

MSIMU WA 2014/15

Simba haikuwahi kufika hata nafasi ya pili katika msimu mzima, lilikuwa jambo jipya kabisa kwa mabingwa hao mara 19 wa zamani kushindwa kabisa kuongoza msimu walau kwa masaa kadhaa tu. Baada ya taji lao la mwisho msimu wa 2011/12 itakumbukwa kuwa msimu uliofuata walimaliza katika nafasi ya 3, wakamaliza nafasi ya nne msimu wa 2013/14, na msimu uliopita walimaliza nafasi ya tatu.

USHINDI WA MECHI 5 MFULULIZO

Baada ya mwendo wa kusuasua mwanzo mwa msimu huu chini ya Muingereza, Dylan Kerry timu hiyo imeonekana kuamka chini ya kaimu kocha mkuu Jackon Mayanja ‘gwiji wa zamani kiuchezaji’ kutoka nchini Uganda. Chini ya Mganda huyo Simba imefanikiwa kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2010 kushinda michezo 6 mfululizo.

Mayanja alianza na ushindi wa 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, kisha akaisimamia timu hiyo kushinda 2-0 mbele ya JKT Ruvu. Kama hiyo haitoshi wakasafiri kwenda Morogoro na kupata ushindi wa 3-0 dhidi ya Burkina Faso FC katika michuano ya kombe la FA. Wakashinda 4-0 dhidi ya African Sports kisha 5-1 dhidi ya JKT Mgambo katika michezo ya ligi kuu.

Jumapili iliyopita walipata ushindi wa 1-0 dhidi ya Kagera Sugar katika uwanja wa Kambarage.

Matokeo hayo mazuri mfululizo yamerejesha ari katika timu na huku wakiwa nyuma kwa alama moja tu dhidi ya vinara Yanga SC, nafasi pekee ya wao kushika usukani ni kuwafunga Stand katika mchezo wa Jumamosi hii kwa kuwa timu za Yanga na Azam FC hazitakuwa na mechi za ligi kuu wikendi hii kutokana na kukabiliwa na michezo ya vilabu Afrika.

MECHI 3 ZILIZOPITA DHIDI YA STAND UNITED

Stand ni timu mpya kabisa katika mpira wa miguu Tanzania bara. Huu ni msimu wao wa pili kucheza ligi hiyo ya juu zaidi nchini baada ya kunusurika kushuka siku ya mwisho ya msimu uliopita baada ya kuishinda Ruvu Shooting ya Pwani iliyoteremka daraja (Shooting tayari wamerejea VPL msimu ujao).

Mechi yao ya kwanza katika ligi kuu dhidi ya Simba ilimalizika kwa sare ya 1-1 katika uwanja Taifa, Dar es Salaam, wakashinda 1-0 katika uwanja wao wa nyumbani (Kambarage.) Mechi yao ya kwanza msimu huu ilimalizika kwa Simba kushinda 1-0 katika uwanja wa Taifa.

Mechi yao ya nne haitakuwa rahisi kwa kuwa kila timu ipo vizuri na timamu kimwili na kiakili. Stand wanashika nafasi ya 5 wakiwa na pointi 29 wakati Simba wataingia uwanjani wakiwa na pointi 42 katika nafasi ya pili ya msimamo.

Itakuwa mechi kali lakini kitendo cha Simba kushindwa kupata ushindi kitakuwa kimewanyima nafasi ya kuongoza ligli.

Salim Mbonde Asisitiza Kiu Ya Ubingwa Wa Tanzania Bara 2015-16
Angalia Orodha Ya Mabondia 10 Bora Kwa Nyakati Zote