Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Frederick Sumaye ameutaja ugonjwa ambao unakitafuna chama hicho kikuu cha upinzani ambao ni tishio kwa chama hicho kuelekea uchaguzi za Serikali za Mitaa mwakani.

Sumaye ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Pwani, amesema kuwa chama hicho hakifanikiwa kushinda uchaguzi endapo vingozi wake watajikita katika kupigania maslahi binafsi, akitoa mfano wa baadhi ya waliokuwa viongozi wa chama hicho ambao walitimka na kuacha nyadhifa zao.

Alisema kuwa sababu kuu itakayowapa ushindi katika uchaguzi ujao ni endapo chama hicho kitajikita katika kupigania maslahi mapana ya wananchi badala ya maslahi binafsi.

Hivi karibuni, kulikuwa na wimbi la madiwani na wabunge wa ngome ya vyama vya upinzani kujiuzulu na kutimkia Chama Cha Mapinduzi ambako walipewa nafasi ya kugombea tena nafasi hiyo.

“Tunapojiandaa na uchaguzi tuzingatie maslahi mapana ya wananchi. Ugonjwa mkubwa niliouona ndani ya chama chetu ni miongoni mwa watu kufikiria maslahi yao binafsi jambo ambalo halitakiwi,” alisema Sumaye katika kikao cha ndani cha Baraza la Uongozi wa ndani.

Sumaye alisema kuwa ifikapo wakati wa uchaguzi, ni vyema chama hicho kikaangalia wanachama ambao walikuwa wanakipigania wakati wote katika kuwapa nafasi za kugombea na kuwaepuka wale ambao hawako pamoja katika kujenga chama lakini huingia wakati ambapo wanataka kugombea nafasi.

Naye Katibu wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mrema alisema kuwa mchakato wa kuwapata watu watakaogombea nafasi mbalimbali za uongozi kuanzia ngazi ya Serikali za Mitaa hadi urais watapitia mchakato wa chama na kutajwa mapema.

Breaking: Mourinho atimuliwa Man United
Jangili asukumwa ndani na kuamriwa kuangalia filamu ya wanyama

Comments

comments