Wanamgambo wa Taliban wamesherekea baada ya Marekani kuondoa vikosi vyake nchini Afghanistan, hatua hiyo imejiri baada ya majuma kadhaa kuchukua  udhibiti wa Serikali iliyokuwa ikiongozwa na Rais Ashraf Ghani.

Milio ya risasi ya sherehe imesikika mji wa Kabul nchini Afghanistan wakati wapiganaji wa Taliban walipodhibiti uwanja wa ndege wa Kabul kabla ya alfajiri, kufuatia kuondoka kwa wanajeshi wa mwisho wa Marekani.

Kuondoka huko kunashiria kumalizika kwa vita vya miaka 20 ambavyo viliwaacha wanamgambo wa Kiislam wakiwa na nguvu kuliko ilivyokuwa mnamo mwaka wa 2001.

Vita hivyo nchini Afghanistan ndivyo vya muda mrefu zaidi kwa Marekani, vikigharimu takriban dola tilioni mbili, na vimemalizika kwa wanamgambo wenye msimamo mkali wa Kiislam kudhibiti eneo zaidi kuliko wakati wa utawala wao uliopita.

Picha za video zilizosambazwa na Taliban zinaonesha wapiganaji wakiingia kenye uwanja huo wa ndege baada ya wanajeshi wa mwisho wa Marekani kuondoka kwa ndege ya C-17, katika kile kinachotajwa na baadhi ya wachambuzi kama kisa cha aibu kwa Washington na washirika wake wa NATO.

“Ni siku ya kihistoria na wakati wa kihistoria, tunajivunia nyakati hizi, kwamba tumeikomboa nchi yetu kutoka kwa nchi zenya nguvu kubwa,” amesema msemaji wa Taliban Zabihullah Mujahid baada ya Wamarekani kuondoka.

Zaidi ya watu 123,000 wameondoka nchini humo kwa kuhofia utawala wa Taliban.

Vyumba 17 vyateketea kwa moto Kagera
Jerry Slaa afungiwa kuingia Bungeni