Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), imetakiwa kuongeza uvunaji wa malisho ya mifugo katika vituo vyake vyote nchini, ili jamii inayowazunguka iweze kujifunza juu ya ulimaji wa hitaji hilo.

Wito huo, umetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo, Tixon Nzunda wakati wa ziara ya kikazi ya siku moja katika kituo cha TALIRI na kampasi ya Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA), Wilayani Mpwapwa, Mkoani Dodoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo, Tixon Nzunda akikagua mifugo wakati wa ziara ya kikazi ya siku moja katika Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Wilaya ya Mpwapwa, Mkoani Dodoma.

Amesema, mbali na jamii inayoishi karibu na vituo vya TALIRI kujifunza juu ya ulimaji wa malisho ya mifugo, pia wanapaswa kujifunza juu ya teknolojia rahisi ya uvunaji wa malisho, pamoja na kufahamishwa utaratibu wa ulimaji, undaaji wa mashamba na uvunaji wa mbegu.

Aidha, ameiasa sekta binafsi kujikita katika biashara ya malisho ya mifugo kwa kuwekeza kwenye vifaa vya uvunaji wa malisho hasa malisho ya asili, ambayo kwasasa ni biashara yenye faida kwani robota moja linauzwa kuanzia Shilingi 4,000 na kuwataka vijana kuchangamkia fursa ya ulimaji wa malisho ya mifugo.

Hata hivyo, katika upande mwingine, Nzunda amewataka Wafanyakazi wa TALIRI na LITA kufanya kazi kutokana na mabadiliko ya mazingira na kuzidi kuboresha utendaji wao wa kazi.

Katika ziara hiyo, Katibu Mkuu Nzunda ameambatana na Mwenyekiti wa bodi ya TALIRI Prof. Sebastian Chenyambuga, Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo Prof. Erick Komba, Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Angello Mwilawa na viongozi wa TALIRI na LITA.

Almasi yetu si laana ni Baraka: Rais Masisi
Bodi ya maji yabaini chanzo kina cha maji kupungua