Serikali ya Tanzania imepewa tuzo 2 za masuala ya Ustawi wa Jamii  pamoja na ushirikishwaji wa wanawake katika ngazi ya maamuzi ya Serikali na Taasisi mbalimbali katika Mkutano wa 27 wa Umoja  wa Nchi za Afrika (AU) uliofanyika hivi karibuni Kigali nchini Rwanda

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi, Augustine Mahiga, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam kuhusu mambo yaliyojadiliwa katika mkutano wa 27 wa Umoja wa nchi za Afrika uliofanyika hivi karibuni Kigali nchini Rwanda.

“Tanzania imetambuliwa na AU kama nchi ambayo kwa miaka 15 sasa  imekua na mikakati mbalimbali  ya kitaifa ya kuzingatia haki za wanawake na kutimiza malengo ya Milenia,”  alisema Balozi Mahiga

Aliongeza kuwa Tanzania ni kati ya nchi tano bora katika bara la Afrika ambazo zimepewa tuzo hizo.

Katika hatua nyingine, Balozi Mahiga amasema kuwa katika mkutano huo wa 27 viongozi wa Afrika walizungumzia mambo mbalimbali ikiwemo  hati ya kusafiria Afrika (passport), ambayo itawezesha watu wa bara hilo kusafiri katika nchi zote za Afrika.

Balozi Mahiga aliongeza kuwa, lengo la kuanza kutumia hati hiyo ya kusafiria kwa nchi za Afrika ni kutoa vikwazo vilivyokuwepo wakati wa kutembelea na kusafiri ndani ya nchi hizo.

 

Aidha, Balozi Maiga amesema kwamba, kutolewa kwa hati ya kusafiria ya Afrika ni ishara ya Umoja na mshikamano, hati hizo zimeanza kutolewa kwa marais na viongozi wa Serikali wa nchi ambazo zilihudhuria mkutano huo. Hati hizo zitatumika kwa kuzingatia sheria za kila nchi.

Bavicha Wajipanga kwa Mkakati Mwingine Kuhusu Mkutano wa CCM
Ripoti Ya Utafiti Utumikishwaji Watoto Yazinduliwa