Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imekifungia kwa miezi mitatu kipindi cha Take One kinachorushwa na Kituo cha runinga cha Clouds TV cha jijini Dar es Salaam baada ya kujiridhisha kuwa kilirusha kipindi chenye maudhui yanayohamasisha ukahaba.

Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, Kaimu mwenyekiti wa kamati ya maudhui ya TCRA, Joseph Mapunda alisema kuwa kipindi hicho kikiongozwa na mtangazaji wake, Zamaradi Mketema kilifanya mahojiano na msichana mmoja kuhusu biashara ya ukahaba aliyodai ameifanya.

Mapunda alisema kuwa kipindi hicho kilirushwa Agosti 9 mwaka huu na kurudiwa kesho yake mchana. Alisema kuwa katika mahojiano hayo, msichana huyo aliyedai kuwa mfanyabiashara ya ukahaba aliwataja wateja wake kwa majina.

Kamati hiyo ilieleza kuwa adhabu hiyo ya kifungo cha miezi mitatu kwa Take One imeanza tangu Jumanne wiki hii.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo alisema kuwa Kamati ilifanya mahojiano na uongozi wa Clouds TV ambao ulikiri kufanya makosa ikiwa ni pamoja na kuhamasisha moja kwa moja biashara ya ukahaba, kushindwa kufanya uhariri wa kutosha wa kipindi, kutozingatia kanuni za uandishi wa habari pamoja na kutosimamia ipasavyo kipindi hicho.

“Ni kweli ninakiri tulikosea kuweka wazi majina ya watu waliotajwa na msichana yule kuwa walikuwa wateja wake. Pia, uhariri wa kipindi haukufanywa kiuweledi,” kamati hiyo ilimkariri mtangazaji wa ‘Take One’, Zamaradi Mketema.

Adhabu hiyo imetolewa na TCRA ikiwa ni miezi michache baada ya kutoa onyo kwa kituo hicho kwa kufanya mahojiano na mtu anayejihusisha na mapenzi ya jinsia moja (shoga) kupitia kipindi hicho cha Take One.

Kubenea apandishwa kizimbani kwa ‘habari za uongo’
Bodi ya CUF yachanika katikati, Lipumba apata watetezi wapya