Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) na klabu ya AFC Eskilstuna inayoshiriki ligi kuu nchini Sweden, Thomas Ulimwengu atalazimika kukaa nje ya uwanja kwa muda wa miezi mitatu akiuguza jeraha la goti.

Ulimwengu aliyejiunga na klabu hiyo mwishoni mwa mwezi Januari alipata majeraha hayo mwezi uliopita hali iliyopelekea akose mechi mbili za kirafiki za Stars dhidi ya Botswana na Burundi licha ya hapo awali kuitwa na kocha Salum Mayanga.

Times FM kupitia kipindi cha Wizara Ya Michezo imezungumza na mshambuliaji huyo kutoka nchini Sweden, ambapo alisema ameelezwa na daktari kuwa atalazimika kukaa nje kwa majuma 12 ili aweze kurejea katika hali yake.

“Niliumia wiki kadhaa zilizopita na ni kama vile nilipona nikaanza mazoezi ndipo nikajitonesha, sasa nimetoka kwa daktari hapa muda huu ameniambia nipumzike kwa miezi mitatu ndipo nitakuwa fit,” alisema Ulimwengu.

Tayari Ulimwengu ambaye alishaanza kuonyesha makeke mazoezini na katika mechi za kirafiki amekosa mechi mbili za ligi kuu nchini humo ambayo imeanza hivi karibuni na majeraha haya yatamfanya akose mechi nyingi zaidi.

Askofu Banzi: Tuungane kupiga vita mtandao wa dawa za kulevya
Mwenyekiti Chama cha Wafanyakazi Kilimanjaro Mahakamani kwa Kugushi Vyeti