Gwiji wa soka nchini Brazil Eduardo Gonçalves de Andrade (Tostao) ameonyesha imani dhidi ya nahodha na mshambuliaji wa timu ya taifa ya nchi hiyo Neymar da Silva Santos Júnior kuelekea fainali za kombe la dunia za mwaka 2018.

Gwiji huyo ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha timu ya taifa ya Brazil kilichoshiriki fainali za kombe la dunia za mwaka 1966 na 1970, amesema Neymar ameonyesha kuwa na ujasiri wa kuwa kiongozi hodari dhidi ya wachezaji wenzake.

Tostao amesema mshambuliaji huyo wa FC Barcelona, huenda akawa mkombozi katika fainali zijazo za fainali za kombe la dunia ambazo zitafanyika nchini Urusi, kutokana na juhudi na maarifa aliyonayo ambayo yameonyesha kuwajenga wachezaji wengine.

Hata hivyo gwiji huyo amekwenda mbali zaidi na kumtabiria Neymar kuwa nahodha mtarajiwa wa kikosi cha Brazil ambaye atakabidhiwa kombe la dunia katika fainali za 2018.

Akitoa sababu za kusema maneno hayo Tostao ametanabaisha kwamba, kikosi cha Brazil cha sasa kina mtazamo tofauti wa kiushindani na hakina uwoga wa kucheza na taifa lolote duniani, hivyo hana shaka na mafanikio  ambayo anatarajiwa kuyaona mwaka 2018.

Image result for Tostao on sky sportsEduardo Gonçalves de Andrade Tostao (kulia) akiwa na Pele

“Kikosi hiki cha Brazil kina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa dunia mwaka 2018, kutokana na kuwa na uwezo mkubwa wa wachezaji ambao wanaongozwa na Neymar, ”

“Wachezaji wanaonyesha kupevuka kimwili na kiakili, jambo ambalo linawafanya wacheze soka kwa malengo ya kuisaidia nchi yao, naamini mwaka 2018 kuna mafanikio yatapatikana.”Alisema Tostao.

Kwa mara ya mwisho Brazil walitwaa ubingwa wa dunia katika fainali za mwaka 2002 zilizofanyika Korea kusini na Japan, na mwaka 2014 lakini walipata aibu kubwa ya kihistoria baada ya kukubali kufungwa mabao 7-1 dhidi ya Ujerumani katika mchezo wa nusu fainali.

 

Arda Turan Aeleza Jiangsu Suning Walivyoshindwa Kumsajili
Baraza la mitihani kuanza kufanya uhakiki wa vyetu kwa watumishi wa Serikalini