Beki wa Kushoto wa Simba SC Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ ameitakia kila la kheri timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ambayo baadae leo Ijumaa (Machi 24) itacheza mchezo wa Mzunguuko watatu wa Kundi F, kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ dhidi ya Uganda.

Taifa Stars itakuwa ugenini nchini Misri ikicheza dhidi ya wenyeji wao The Cranes iliyochagua mchezo huo kupigwa katika mji wa Ismailia kwenye Uwanja wa Suez Canal, kufuatia Uganda kukosa viwanja vinavyokidhi vigezo vya Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.

Tshabalala amesema Taifa Stars inakabiliwa na mchezo mgumu kwa sababu Uganda ‘The Cranes’ imekuwa na timu nzuri ambayo mara kwa mara imekua ikisumbua katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Beki huyo amesema anakiamini kikosi cha Taifa Stars ambacho kimekuwa kambini nchini Misri tangu mwishoni mwa juma lililopita, hivyo amekiri atakuwa pamoja na kikosi hicho katika muda wote wa dakika 90 za mchezo wa leo Ijumaa.

“Tunakwenda kwenye mechi ngumu. Uganda wana timu nzuri, lakini nawaamini wachezaji wenzangu.Ugumu wa mchezo huu ni kwa sababu tunafahamiana. Hii ni kama Derby, kupigwa na jirani yako kunakuwa na ishu nyingine”

“Najua tunakwenda kwenye mechi ngumu, lakini naliamini jeshi langu.Nitakuwepo kiwanjani Jumanne katika mchezo wa marudiano kwa ajili ya kuwaunga mkono wenzangu” amesema Tshabalala

Taifa Stars inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa Kundi F ikiwa na alama 01 sawa na Uganda inayoburuza mkia, huku Algeria ikiongoza kwa kufikisha alama 06 na Niger ipo nafasi ya pili kwa kuwa na alama 02.

Chipolopolo yaiwahi Lesotho Johannesburg
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Machi 24, 2023