Utafiti uliofanywa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Twaweza umeonesha kuwa asilimia 60 ya Watanzania walioshiriki utafiti huo wanaunga mkono uamuzi wa Serikali ya awamu ya Tano kupiga marufuku mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.

Hayo yamebainishwa jana jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa matokeo ya utafiti huo uliohusisha sampuli ya watu 1,602 kati ya mwezi Agosti 23 na 29 mwaka huu.

Akisoma sehemu ya matokeo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, idan Eyakuze alisema imebainika kuwa asilimia 49 wamesema kuwa mikutano baada ya uchaguzi hupelekea kukwamisha maendeleo huku asilimia 47 wakitaka vyama vya siasa viruhusiwe kuendelea kufanya mikutano yao bila pingamizi.

Hata hivyo, utafiti huo ulibainisha kuwa kati ya wahojiwa waliounga mkono marufuku ya mikutano ya vyama vya siasa, asilimia 70 walikuwa wanachama wa Chaama Cha Mapinduzi na asilimia 33 walikuwa wafuasi wa vyama vya upinzani.

Aidha, utafiti huo ulionesha kuwa asilimia 29 ya wahojiwa walionesha nia ya kushiriki katika maandamano yaliyoitishwa na vyama vya siasa nchini huku asilimia 50 walisema hawako tayari kushiriki.

Akizungumzia hali ya demokrasia nchini, Eyakuze alisema kuwa watanzania wengi wanaridhishwa na uwepo wa demokrasia na wanapingana na hoja ya kuwa Rais John Magufuli ni dikteta.

“Watanzania wengi wanauunga mkono mfumo wa demokrasia ya vyama vingi na uhuru wa kukusanyika  na kutoa maoni,” alisema. “Idadi kubwa ya wananchi hawakubaliani na kauli inayosema Rais Magufuli ni dikteta,” aliongeza Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Twaweza.

Arsene Wenger Apambanishwa Na Eddie Howe
Waziri Mkuu kuhamia Dodoma kesho