Maelfu ya vikosi vya jeshi la Namibia yamelazimika kupumzishwa kutokana na ukata uliolikumba jeshi hilo kiasi cha kukosa fedha ya chakula pamoja na kulipia bili za maji na umeme kwa baadhi ya maeneo.

Kwa mujibu wa gazeti la Namibia, Kambi saba za jeshi zimeathirika na ukata huo na kwamba baadhi ya wanajeshi ambao walikuwa likizo wamelazimika kurejeshwa ili kupunguza posho za likizo hizo.

Wizara ya ulinzi ya nchi hiyo imekubwa na mtikisiko wa kifedha baada ya serikali kupitisha panga kwenye bajeti kwa lengo la kupunguza matumizi.

Imeelezwa pia kuwa Rais Hage Geingob amepiga marufuku safari za maafisa wa Serikali nje ya nchi.

“Hakutakuwa na safari yoyote ya nje ya nchi kwa mawaziri, manaibu waziri na viongozi wengine wa kisiasa, hadi itakapofikia mwishoni mwa mwezi Februari,” limeeleza tamko la Ikulu.

Rais Geingob pia aliacha kutumia ndege maalum ya rais, na aliamua kusafiri hivi karibuni kwenda kwenye mkutano wa Umoja wa Afrika nchini Ethiopia kwa kutumia ndege ya kawaida ya biashara chini ya mpangilio maalum.

Msemaji wa Ikulu, Albertus Aochamub ameliambia shirika la habari la AFP kuwa Rais Geingob atafanya safari za nje zenye uzito zaidi na atakuwa na watu wachache zaidi wa kumsindikiza.

TLS yamuunga mkono Magufuli
Serikali yafanya mabadiliko TTCL