Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Stephanie Williams amelaani uvamizi wa majengo ya bunge uliofanywa na waandamanaji wenye hasira na kusema kuwa vitendo vya uharibifu havitakubalika.

Waandamanaji hao walivamia jengo la bunge mjini Tobruk, wakipinga kupanda kwa gharama za maisha na kushindwa kwa wanasiasa kukubaliana juu ya tarehe ya uchaguzi uliocheleweshwa.

Maandamano pia yalifanyika katika miji mingine ya Tripoli, Benghazi na Misrata, ambapo katika eneo hilo la Bunge waliyachoma moto majengo kadhaa.

Baadhi ya waandamanaji nchini Libya wanaopinga kucheleweshwa kwa uchaguzi na kupanda kwa gharama za maisha. Picha: REUTERS

Itakumbukwa kuwa, Libya imetumbukia katika machafuko tangu vuguvugu lililoungwa mkono na Jumuiya ya kujihami NATO, kwa kumwondoa madarakani Rais wa muda mrefu Muamar Gadaffi mwaka 2011.

Kwa miaka kadhaa, nchi hiyo imegawanyika katika tawala mbili hasimu za upande wa mashariki na magharibi, zote zikiungwa mkono na makundi tofauti ya wapiganaji na Serikali za kigeni.

Rasmi Waziri aifikisha tuzo kwa Rais mstaafu
Wanasiasa kuelimisha jamii madhara dawa za kulevya