Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kusimamia ulinzi wa watoto na kupinga ukatili dhidi yao huku akisisitiza kwamba ni lazima kila mtoto wa Kitanzania alindwe na atunzwe.

Ameyasema hayo leo Desemba 4, 2021 wakati akizungumza na wadau mbalimbali walioshiriki maadhimisho ya miaka 75 ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto (UNICEF) kwenye ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.

“Lazima mtoto wa Kitanzania alindwe, atunzwe. Mtoto wa mwenzio ni wako. Kama kuna Mtanzania yoyote anatenda ukatili na hamtunzi mtoto, lazima achukuliwe hatua za kisheria. Kwenda shule ni lazima kwa mtoto wa Kitanzania. Asipoenda shule, ukamtuma kuuza maandazi stendi, tukimkamata tutakushtaki wewe mzazi au mlezi,” Amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Aidha Waziri Mkuu Majaliwa amepongeza hoja zilizoibuliwa na watoto na vijana balehe kwenye mjadala uliokuwa mubashara katika mkutano huo, Waziri Mkuu amewapongeza vijana hao watano kutoka mikoa ya Dodoma, Mwanza, Arusha, Dar es Salaam na Zanzibar kwa kuwasilisha kwa uwazi na ujasiri hoja hizo.

Watoto wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza katika Maadhimisho ya Miaka 75 ya Shirika la Kuwahudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) kwenye ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma

Kati ya zilizowasilisha ni kutaka Serikali iongeze bajeti kwenye ajira za walimu ili kukabiliana na upungufu uliopo; kuboresha miundombinu ya shule ikiwemo maji; kuboresha mitaala ya elimu ili iendane na soko la ajira; kuondolewa kwa adhabu ya viboko, kupatiwa taarifa sahihi za elimu ya afya na kupewa fursa ya kuonesha vipaji vyao na kutambuliwa.

Akifafanua hoja hizo, Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imeshaanza kutekeleza baadhi ya mambo kama vile kuajiri walimu 6,900 (hadi Juni, 2021), kujenga maabara, kujenga mabweni ili watoto wanaokaa mbali na shule wasipate shida, kutoa sh. bilioni 20.5 kila mwezi za elimu msingi bila ada ili kuwawezesha vijana wasome bila usumbufu wa michango kwa wazazi na kuboresha miundombinu ya kujifunzia na ya kufundishia.

Kuhusu suala la kupata taarifa na huduma rafiki za afya ya uzazi kwa vijana, Waziri Mkuu amesisitiza wizara husika zihakikishe kuwa elimu sahihi yenye kuzingatia umri wa mtoto, mila na tamaduni zetu inatolewa katika ngazi zote.

Kuhusu suala la adhabu ya viboko shuleni na athari zake kwa watoto, Waziri Mkuu amesema jambo hilo linahitaji mjadala mpana utakaohusisha wadau wote kwa sababu lina changamoto  nyingi zikiwemo za mfumo wa malezi, maadili na tamaduni za makabila tofauti.

Naye Mwakilishi Mkazi wa UNICEF hapa nchini, Bi. Shalini Bahuguna amesema miaka 75 iliyopita, isingetarajiwa kwamba watoto wanaweza kukaa jukwaa moja na viongozi wakuu wa nchi na kutoa maoni lakini kwa sasa jambo hilo linawezekana.

Ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuwa miongoni mwa nchi za mwanzo kusaini Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Mtoto na akaomba viongozi waliopo madarakani wawasikilize watoto na kufanyia kazi maoni wanayoyatoa ili kuboresha maisha ya watoto na Tanzania kwa ujumla.

STAMICO, Suness Ltd zasaini mkataba wa mashirikiano
Wanaoiba vifaa vya ujenzi BRT waonywa