Maelezo ya mshtakiwa wa pili katika kesi ya uhujumu uchumi ya Freeman Mbowe na Wenzake, Adam Kasekwa yanasema Freeman Mbowe alipanga kumdhuru aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya.

Katika ushahidi alioutoa leo, Oktoba 26, 2021 katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Ramadhani Kingai amesoma maelezo ya mtuhumiwa huyo kwamba Mbowe alisema Sabaya anahatarisha nafasi yake ya kuendelea kuwa mbunge wa Hai.

“Mbowe alituelekeza tufuatilie nyendo zake na tumdhuru kwa spray ya sumu. Ling’wenya alifuatilia mtu wa kupata sumu. Tarehe 27 tulirudi Dar na magari mawili pamoja na Mbowe na mlinzi wake.

“Baada ya kufika Dar tulifikishwa Mikocheni mimi na Ling’wenya tulipewa Sh200,000 tujiandae.Baadaye tulipewa nauli turudi Moshi. Agosti Mosi saa 11 alfajiri Mbowe alituita akasema tutekeleze maelekezo ya kumdhuru Sabaya.

“Alituelekeza baada ya kazi ya Sabaya turudi Dar kutekeleza kazi nyingine nyeti kulipua vituo vya mafuta na kushinikiza maandamano ili Serikaki ionekane imeshindwa maana inatuchukia sisi wapinzani”.

“Tulikamatwa na askari tukituhumiwa kukutwa na dawa za kulevya na kupanga njama za ugaidi. Tuhuma hizo ni za kweli na pia kukutwa na silaha ni za kweli na nilikutwa na simu yangu ya Itel”.

Katika hatua nyingine Kamanda wa Polisi Kinondoni, Ramadhani Kingai amesema walichelewa kumkamata Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kwa sababu walitaka kujiridhisha uhusika wake katika tuhuma za kupanga kutekeleza ugaidi.

Katika ushahidi wake leo Jumanne Oktoba 26, 2021 Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Kingai ameieleza mahakama pia kuwa walichelewa kumkamata Mbowe kwa sababu upelelezi dhidi ya tuhuma zilizomkabili ulikuwa ukiendelea.

“Taarifa za kuhusika zilikuwa za mwanzo tangu mwezi Julai 2020. Baada ya kukamilisha na kujiridhisha na upelelezi wetu ndipo tulimkamata kuhusiana na tuhuma hizi” amesema Kingai.

“Kulingana na taarifa kutoka kwa Luteni Urio na vitendo vilivyokuwa vimepangwa, kudhuru viongozi wa Serikali, kufanya vurugu eneo la masoko, kulipua vituo vya mafuta kukata miti kwenye Highway hasa njia ya Iringa ndio maana tulifungua jalada la Makosa ya ugaidi.

Hivi ni vitendo ambavyo vingeweza kuleta taharuki na hofu kwa wananchi kuona hawako salama na vilileta tafsiri ya kosa la kigaidi” Amesema RPC Kingai

Mwanamke aliyejifungua watoto 9 awaonyesha sura zao
Rais Samia amtembelea Waziri mstaafu Lowassa