Uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme, iliyoungwa katika mfumo wa gridi ya Taifa umeongezeka na kufikia megawati 1,777.05 mwezi Desemba 2022 sawa na ongezeko la asilimia 4.87, ikilinganishwa na megawati 1,694.55 zilizokuwepo hadi kufikia mwezi Septemba 2022.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nishati, Januari Makamba jijini Dodoma wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya Wizara kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati kuhusu utekelezaji wa Bajeti kwa kipindi cha mwezi Julai-Desemba, 2022.

Amesema, katika kipindi cha mwezi Julai-Desemba 2022 jumla ya futi za ujazo milioni 38,172 za gesi asilia zilizalishwa katika vitalu vya Songosongo na Mnazi Bay, na umeongezeka kwa asilimia 27 ikilinganishwa na kipindi Julai-Desemba, mwaka 2021 zilipozalishwa futi za ujazo 29,996.

Waziri wa Nishati, Januari Makamba.

Aidha, Makamba ameongeza kuwa ongezeko la uwezo wa mitambo hiyo ya kuzalisha umeme iliyoungwa katika mfumo wa gridi limetokana kuingizwa katika Gridi ya Taifa megawati 90 za umeme zinazozalishwa katika Kituo cha Kinyerezi I Extension.

Ameongeza kuwa, uwezo wa kuzalisha umeme kwa mitambo ambayo haijaunganishwa katika gridi ya Taifa umefikia megawati 39.302 na hivyo kufanya jumla ya uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme nchini kufikia megawati 1,816.352 ikilinganishwa na megawati 1,733.38 zilizokuwepo mwaka 2021/2022 sawa na ongezeko la asilimia 4.89.

Hersi afunguka usajili Dirisha Dogo
Mbowe akana kulamba asali mbele ya hadhara