Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli ameitaka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kutoa kipaumbele katika uwekezaji wa miundombinu ya mawasiliano kwa Kampuni ya Mawasiliano Nchini (TTCL) ili iweze kumiliki idadi kubwa ya minara ya mawasiliano ya simu na kumudu ushindani wa soko la mawasiliano nchini.

Ameyasema hayo jijini Dar es salaam wakati wa hafla ya upokeaji wa Gawio la Serikali la Tsh. Bilioni 2.1 kutoka TTCL ambapo amesema kuwa njia pekee ya kuiendeleza TTCL ni kwa Viongozi na Watendaji wa Serikali kuwa na moyo wa uzalendo wa kusimamia rasilimali za umma.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli alisema TTCL imekuwa ikitumia kiasi cha Tsh Milioni 700-800 kila mwezi kwa ajili ya kukodisha minara ya mawasiliano, wakati Serikali ina mfuko wa mawasiliano kwa wote (UCSAF) unaotoa ruzuku kwa makampuni mbalimbali ya mawasiliano kwa ajili ya kujiwekeza katika miundombinu ikiwemo minara ya mawasiliano maeneo mbalimbali nchini.

“Hili la TTCL kukopa minara katika makampuni mengine halikubaliki, Serikali ina mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF) ambao wanatoa ruzuku kwa makampuni mengine ya simu lazima tulitazame upya, nataka sasa TTCL tuwape mitaji ya kutosha ili kuhakikisha kuwa linaendelea kupanua huduma zake kwa Watanzania wengi zaidi,” amesema Rais Magufuli.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba amesema kuwa TTCL imeendelea kupiga hatua kubwa zaidi katika utoaji wa huduma ya mawasiliano nchini ambapo katika mwaka 2018/19, shirika hilo limeweza kupata faida ya Tsh Bilioni 8.3 ambapo kiasi cha Tsh Bilioni 2.1 imetoa gawio kwa Serikali.

“Katika mwaka 2017/18, tulitoa Tsh Bilioni 1.5, lakini kwa mwaka huu tumetoa Tsh Bilioni 2.1 ikiwa ni ongezeko la Tsh Milioni 600, hii imetokana na kuongezeka kwa makusanyo ya mapato yetu kutoka Bilioni 119 mwaka 2017/18 hadi kufikia Bilioni 167 mwaka 2018/19,”amesema Kindamba.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL, Mhandisi Omary Nundu ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kutokana na uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa kwani katika kipindi cha miaka mitatu, shirika hilo limeweza kupata mafanikio makubwa kutokana na maono na dhamira ya Rais Dkt. John Magufuli kwa shirika hilo.

Pierre atimiza ahadi yake kwa DC Jokate, ashusha madawati
DC apiga marufuku gari ya abiria kusimamishwa mara mbili ndani ya wilaya yake

Comments

comments