Wafanyabiashara ndogo ndogo (Machinga) wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala wameiomba Serikali kuwatengezea utaratibu maalumu ili waweze kutambulika na kufanyabiashara zao kwa uhuru zaidi na kulipa kodi ili waweze kuchangia pato la taifa na kuleta maendeleo katika jamii.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa wamachinga, Steven Lusinde katika mazungumzo maalum na Dar24 ambpo ameeleza kuwa kilio chao kikubwa ni kurasmishwa kwa biashara zao ili watambulike na Serikali wawe na usalama katika biashara zao.

Amesema kama watatengenezewa utaratibu maalum, Serikali itakusanya mapato makubwa ambayo kwa sasa yanapotea kwani wapo wengi sana na wanayonia ya kutambuliwa kama wafanyabiashara na kulipa kodi kwa Serikali.

Lusinde amesema kuwa, viongozi wengi wamekuwa wakiwatumia wakati wa Kampeni kwaajili ya kupata kura, lakini baada ya uchaguzi hali huendelea kuwa ileile ya manyanyaso yanayowasababishia kupoteza heshima katika familia zao na jamii kwa ujumla.

Aidha, ametoa pongezi na kumshukuru Rais, DK. john Pombe Magufuli kwa kuwakumbuka hali iliyosababisha sasa wanafanya biashara zao vizuri japo kuna viongozi wengine bado wanawakandamiza.

“Mimi huwa nawaambia wenzangu kuwa Magufuli ni Musa kwa maana kwamba watu wa dini wanajua alipewa fimbo akapiga bahari ya Shamu, kwenda kuwaokoa wana wa Israel, huyu kaja kuwaokoa watanzania hasa sisi wanyonge,” amesema Lusinde.

Lusinde ameongeza kuwa Machinga wana nia njema ya kujikwamua na wako tayari kushirikiana na Serikali ili kuweza kufikia malengo ya kila mmoja kwa upande wa Serikali na machinga.

Vijiji 53 Njombe kupatiwa huduma ya maji
NEC Yatoa neno kuelekea uchaguzi mdogo wa madiwani na ubunge